Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

Anwani za Makazi na Urithi wa Taifa: Wageni wa Kongamano Watembelea Makumbusho


Na Mwandishi Wetu, WMTH–DSM

Washiriki wa Kongamano la Mwaka la Anwani za Makazi na Maonesho ya Teknolojia za Huduma za Posta kutoka nchi mbalimbali wametembelea Makumbusho ya Taifa ikiwa ni sehemu ya ziara maalum ya kutembelea vivutio vya kihistoria na kujifunza kuhusu urithi wa taifa.

Washiriki hao walifanya ziara hiyo tarehe 07 Februari, 2026 na kujifunza historia ya Tanzania pamoja na kuona na kufahamu mabaki mbalimbali ya kihistoria yaliyohifadhiwa katika Makumbusho ya Taifa.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Mawasiliano, Mhandisi Edith Turuka alisema kuwa lengo la ziara hiyo lilikuwa ni kutangaza utalii wa Nchi yetu pamoja na kuonesha namna urithi wa kihistoria unavyohusiana na maendeleo ya mfumo wa anwani za makazi. 

Mhandisi Turuka aliongeza kuwa miongoni mwa njia zinazotumika katika utoaji wa majina ya mitaa ni kutumia majina ya watu mashuhuri wa kihistoria na kitaifa, akitaja mifano ya Shaaban Robert na Bibi Titi Mohamed. 

Wageni hao wameonesha kufurahishwa na vivutio vya kihistoria vilivyohifadhiwa katika Makumbusho ya Taifa na wameishukuru Serikali pamoja na Kamati ya Maandalizi ya Kongamano kwa kutambua umuhimu wa kuwapatia wageni fursa ya kutembelea Makumbusho hayo.


#TACPA2026
#AnwaniZaMakazi
#DigitalTanzania
#AddressingSystem
#PostalTechnology
#SmartAddressing