Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

Wadau Wajadili Maboresho ya Mfumo wa Anwani za Makazi


Na Mwandishi Wetu, WMTH–DSM

Mkurugenzi wa Mawasiliano kutoka Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Bw. Mulembwa Munaku, ameongoza kikao cha wadau kujadili kuhusu utekelezaji wa mifumo ya Anwani za Makazi katika nchi mbalimbali, kwa lengo la kuimarisha mfumo wa anwani za makazi nchini Tanzania ili kuchochea ukuaji jumuishi.

Mjadala huo uliofanyika leo, Februari 07, 2026, ni miongoni mwa shughuli za Kongamano la Mwaka la Anwani za Makazi na Maonesho ya Teknolojia ya Huduma za Posta ambalo ni sehemu ya Maadhimisho ya Wiki ya Anwani za Makazi kwa mwaka 2026.

Akizungumza katika mjadala huo, Bw. Munaku alisema kuwa ushirikiano wa kikanda katika mifumo ya anwani za makazi ni wa umuhimu mkubwa, hususan katika muktadha wa ongezeko la biashara, usafirishaji wa bidhaa, pamoja na utoaji wa huduma kati ya nchi za Afrika. 


Aliongeza kuwa kwa sasa mifumo ya anwani za makazi mara nyingi huishia ndani ya mipaka ya kitaifa, hali inayopunguza ufanisi wa biashara, utoaji wa huduma za dharura, pamoja na huduma nyingine muhimu. Katika Kongamano hilo wajumbe walibadilishana uzoefu kutoka nchi zao na kutoa mapendekezo mbalimbali kuhusu namna bora ya kuboresha na kuimarisha mfumo wa Anwani za Makazi nchini Tanzania.

#TACPA2026