Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

Mfumo wa Anwani za Makazi: Funguo za Maendeleo ya Jamii na Uchumi wa Kidijitali


Na Mwandishi Wetu, WMTH-DAR ES SALAAM

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mheshimiwa Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki, amesema kuwa Mfumo wa Anwani za Makazi umeleta mabadiliko makubwa katika kuboresha huduma za kijamii na kiuchumi nchini Tanzania.

Waziri Kairuki ameyasema hayo leo akimwakilisha Mheshimiwa Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, katika Kilele cha Maadhimisho ya Wiki ya Anwani za Makazi kilichofanyika tarehe 08 Februari, 2026 jijini Dar es Salaam.

Alieleza kuwa Mfumo wa Anwani za Makazi umewezesha utambuzi sahihi wa maeneo ya makazi, ofisi, biashara, na maeneo mengine muhimu kwa utendaji wa shughuli mbalimbali. Huku akisisitiza kuwa Mfumo huo ni nyenzo muhimu inayoimarisha upatikanaji wa huduma, kurahisisha ukusanyaji wa mapato, na kufanikisha biashara mtandaoni (e-commerce), ikichangia masuala ya usalama.

“Mfumo wa Anwani za Makazi umewezesha Serikali kufuatilia na kuboresha huduma kwa wananchi kwa usahihi na kwa wakati, hivyo kuleta tija katika utoaji wa huduma mbalimbali”,
alisema Waziri Kairuki.

Pia, Waziri Kairuki alitoa pongezi kwa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa kutekeleza Mpango wa kuratibu upatikanaji wa vishikwambi kwa watendaji wa kata, mitaa, shehia, na vijiji kote nchini. Alibainisha kwamba mahitaji ya vishikwambi ni 21,872, lakini hadi sasa vishikwambi 3,482 vimepatikana, na leo anavikabidhi kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu.

“Pongezi nyingi kwa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa kutekeleza kwa vitendo dhamira ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan katika uzinduzi wa Operesheni Anwani za Makazi, ambayo ni muhimu kwa maendeleo ya taifa letu,” alisisitiza Waziri Kairuki.

Maadhimisho ya Wiki ya Anwani za Makazi kwa mwaka 2026 yalianza tarehe 2 Februari, 2026 kwa shughuli mbalimbali ikiwemo Elimu kwa Umma, Kongamano la Anwani za Makazi na Maonesho ya Teknolojia za Huduma za Posta pamoja na maonesho ya Taasisi mbalimbali yaliyohitimishwa leo, tarehe 8 Februari 2026, katika hafla iliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), Jijini Dar es Salaam.

#TACPA2026