Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

WAFANYAKAZI WA POSTA WATAKIWA KUWA NA UBUNIFU WENYE TIJA



Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt. Jim Yonazi amewataka wafanyakazi wa Shirika la Posta Tanzania kuwa na ubunifu utakaoleta tija kwenye Shirika na Taifa kwa ujumla.
 
Ameyasema hayo leo tarehe 19 Agosti, 2022 wakati wa hafla ya kuwapongeza viongozi pamoja na wafanyakazi hodari wa Shirika la Posta katika Makao Makuu ya Shirika hilo, jijini Dar es Salaam.
 
Akizungumza katika hafla hiyo Dkt. Yonazi amesema, bidii na ubunifu ndiyo njia pekee itakayoliwezesha Shirika kufika mbali zaidi kiutendaji na ndiyo kupelekea kuongezeka kwa mapato ya Shirika yatakayoleta tija kwa Taifa
 
Aidha, Katibu Mkuu amewapongeza viongozi na wafanyakazi hodari wa Shirika hilo kwani juhudi na bidii ndiyo iliyowapelekea kupata nafasi hiyo. Hata hivyo, amelitaka Shirika kuwazingatia wafanyakazi wenye nafasi za chini ambao ndiyo wanaowawezesha Viongozi kuonekana kufanya vizuri katika utendaji wao
 
Vilevile, Dkt. Yonazi ametumia hafla hiyo kulipongeza Shirika la Posta kwa jitihada zake mbalimbali za kuendelea kuboresha huduma zake ili kuendana na maendeleo ya Teknolojia Pamoja na mahitaji ya wananchi.
 
Sambamba na hilo Katibu Mkuu Dkt. Yonazi ametoa malekezo kwa Shirika kuhakikisha linaweka kigezo cha Ubunifu wa Biashara Mpakani (Cross Border Business) kwa Viongozi na wafanyakazi ili kuwahamasisha wafanyakazi wa Posta kuongeza bidii katika kutafuta fursa za kibiashara mpakani mwa Tanzania.
 
Naye kwa upande wake Postamasta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania Ndg. Macrice Mbodo amemshukuru Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt. Jim Yonazi kwa kufika katika hafla hiyo na kuahidi Shirika litaendelea kuongeza bidii katika utendaji wake ili kuendelea kuwapatia wananchi huduma bora na zinazoendana na mahitaji yao.