Habari
WADAU WASHIRIKI KUTOA MAONI YA KUBORESHA MKAKATI WA TAIFA WA INTANETI YA KASI
Na Mwandishi Wetu – WMTH, Dar es Salaam
Wadau wa Sekta ya Mawasiliano, Taasisi za Umma na Sekta Binafsi wameshiriki kikao kazi na kutoa maoni ya Rasimu Iliyoboreshwa ya Mkakati wa Taifa wa Intaneti ya Kasi (Updated Tanzania National Broadband Strategy 2026/2027–2030/2031) kabla ya kuanza kwa utekelezaji wake.
Kikao kazi hicho kimefanyika tarehe 8 Juni, 2026, kwa lengo la kuhakikisha mkakati huo unazingatia maoni ya wadau mbalimbali kabla ya kukamilishwa na kuanza kutekelezwa. Ushirikishwaji huo unalenga kuhakikisha mkakati unakidhi mahitaji ya sasa na ya baadae ya maendeleo ya Sekta ya Mawasiliano na Teknolojia za kidigitali nchini.
Vilevile, wadau walitoa maoni kwenye maeneo mbalimbali ya kimkakati yaliyobainishwa katika rasimu hiyo, ikiwemo mfumo wa utekelezaji, ufuatiliaji na tathmini ya mkakati, ujenzi wa uwezo na uhamasishaji wa umma, maudhui, mifumo na huduma za kidigitali, pamoja na utawala, sera, sheria na mifumo ya udhibiti wa sekta.
Maeneo mengine yaliyopewa kipaumbele ni ubunifu, ulinzi wa data, usalama wa mtandao na ushirikishwaji wa kijinsia katika matumizi ya huduma na fursa za kidigitali, ikiwa ni sehemu ya kuhakikisha maendeleo ya kidigitali yanawanufaisha wananchi wote kwa usawa.
Aidha, wadau wameeleza kuwa utekelezaji madhubuti wa mkakati huo utaongeza upatikanaji na matumizi ya huduma za intaneti ya kasi na kuimarisha uwekezaji katika miundombinu ya mawasiliano, kuchochea ubunifu wa kiteknolojia na kupanua fursa za wananchi kushiriki kikamilifu katika uchumi wa kidigitali.
Mkakati wa Taifa wa Intaneti ya Kasi unatarajiwa kuwa nyenzo muhimu katika kuleta mageuzi ya kidigitali nchini na kuchangia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
