Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

Wadau Wakutana  Kuweka Msingi wa Upimaji wa Mchango wa Uchumi wa Kidijitali Tanzania


Na Mwandishi Wetu - Dodoma.

 

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Bw. Mohammed Khamis Abdulla amesema kuwa uwepo wa Akaunti ya Uchumi wa Kidijitali unalenga kuwezesha upatikanaji wa takwimu sahihi zitakazopima kwa ufanisi mchango wa sekta ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika ukuaji wa uchumi na maendeleo ya nchi kwa ujumla.

 

Bw. Abdulla ametoa kauli hiyo tarehe 24 Juni, 2026 akifungua kikao cha kujadili kuhusu maandalizi ya uanzishwaji wa Akaunti ya Uchumi wa Kidigitali.(Digital Economy Satellite Account - DESA) huku akiongeza kuwa mafanikio ya mradi huo yanategemea ushirikiano wa karibu kati ya Serikali na wadau mbalimbali ili kuhakikisha malengo yaliyowekwa yanafikiwa kwa wakati.

 

Akiwasilisha taarifa ya maendeleo ya maandalizi ya akaunti hiyo, Mkurugenzi Msaidizi wa Sehemu ya Sera, Tafiti na Ubunifu, kutoka Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Bw. Hamimu Kachume, amesema kuwa hadi kufikia mwaka jana ukusanyaji wa taarifa muhimu kwa ajili ya utekelezaji wa Akaunti ya DESA ulikuwa umefikia asilimia 90.

 

 

Kikao hicho kilihudhuriwa na Menejimenti ya Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari pamoja na Wakuu wa Taasisi za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), wawakilishi kutoka taasisi mbalimbali za Serikali na sekta binafsi ambao walipata fursa ya kuchangia mijadala, kuuliza maswali na kutoa mapendekezo yatakayosaidia kuimarisha utekelezaji wa mradi huo, unaotarajiwa kuwa nyenzo muhimu katika kupima na kuonesha mchango wa uchumi wa kidijitali katika maendeleo ya Tanzania.