Habari
Wadau Wakutana Dodoma Kuainisha Mahitaji ya Mradi wa Miji Janja nchini.
Kikao Kazi cha Kuainisha Mahitaji ya Mradi wa Upembuzi Yakinifu wa Miji Janja (Smart Cities Feasibility Study Project) kimefanyika kwa mafanikio katika Ukumbi uliopo katika Ofisi za Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mtumba jijini Dodoma, leo 19 Machi 2026, kikikutanisha wadau mbalimbali kutoka wizara, taasisi za umma pamoja na halmashauri za mikoa tofauti nchini.
Akizungumza Mwenyekiti wa kikao kazi hicho, Bw. Baltazari Kibola alisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa karibu baina ya wadau wote katika kuhakikisha mradi huo unatekelezwa kwa ufanisi na kuzingatia mahitaji halisi ya wananchi.
Ameeleza kuwa, maendeleo ya miji janja yanahitaji mipango madhubuti inayochanganya teknolojia ya kisasa na huduma bora za kijamii ili kuboresha maisha ya wananchi.
Wajumbe wamepata fursa ya kuchangia maoni yao, kubainisha changamoto zilizopo katika miji ya sasa pamoja na kutoa mapendekezo ya namna bora ya kuboresha miundombinu ya TEHAMA, usafiri, nishati na huduma nyingine muhimu. Michango hiyo inalenga kusaidia maandalizi ya upembuzi yakinifu utakaoweka msingi imara wa utekelezaji wa mradi wa miji janja nchini.
Kikao hiki kina lengo la kuweka msingi wa maendeleo ya miji yenye matumizi ya teknolojia ya kisasa kama ilivyoainishwa katika DIRA ya maendeleo ya Taifa 2050 yatakayorahisisha upatikanaji wa huduma muhimu kama afya, elimu, usafiri na usalama. Aidha, utekelezaji wa mradi huu unatarajiwa kuongeza ufanisi wa huduma za umma, kukuza uchumi wa ndani na kuboresha ubora wa maisha ya wananchi kwa ujumla.
