Habari
Wadau kutoka CEBOT Wajadili Mustakabali wa TEHAMA na AI Tanzania
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Bw. Mohammed Khamis Abdulla, amekutana na kufanya mazungumzo na ujumbe kutoka Baraza la Bodi ya Soko la Kubadilishana Biashara (Council Exchange Board of Trade - CEBOT) ya Marekani tarehe 25 Machi, 2026 katika Ofisi za Wizara zilizopo Mji wa Serikali, Dodoma.
Katika mazungumzo hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa CEBOT, Bw. Karl Cureton, pamoja na ujumbe wake walieleza kwa kina hali ya ushirikiano wa kiteknolojia kati ya CEBOT, Taasisi ya Teknolojia ya Dar es Salaam (Dar es Salaam Institute of Technology – DIT) na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA).
Wadau hao walisema kuwa ziara yao inalenga kuipatia Wizara taarifa kuhusu maendeleo ya ushirikiano huo, kwa kuzingatia kuwa Wizara ndiyo yenye dhamana ya kusimamia masuala ya TEHAMA nchini. Ushirikiano huo unakusudia kuimarisha matumizi ya Akili Unde (AI) nchini Tanzania, na kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha maarifa ya AI barani Afrika (AI Knowledge Hub), kupitia makampuni tanzu ya CEBOT.
Bw. Abdulla amewashukuru wadau na kuwaahidi kuwa wizara itawapa ushirikiano huku akieleza kuwa tayari Tanzania imepiga hatua kubwa katika masuala ya AI ikiwa ni pamoja na ukamilishaji wa Mkakati wa Akili Unde utakaoweka usimamizi mzuri wa teknolojia hiyo.
Aidha, Bw. Abdulla aliwakaribisha wadau hao wa CEBOT kuongeza ushirikiano katika ufadhili wa Mafunzo ya Teknolojia zinazoibukiwa kwa Wakufunzi kutoka Tanzania watakoenda kufundisha katika Chuo Mahiri cha TEHAMA kinachotarajiwa kujengwa katika Eneo la Nala, mkoani Dodoma.
