Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

VIJANA WATAKIWA KUCHANGIA MAWAZO YAO KATIKA MAAMUZI MAKUBWA YA NCHI ILI KUPATA MAAMUZI BORA


Vijana wametakiwa kufuatililia shughuli mbalimbali zinazofanywa na Serikali ikiwemo Mikutano ya Bunge ili kujua maamuzi yanayofanyika na kuweza kuchangia mawazo yao kwenye maamuzi hayo.

 

Hayo yameelezwa na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye (Mb) wakati akizungumza katika hafla ya kukabidhi tuzo kwa wakurugenzi vijana wa Afrika iliyofanyika katika ukumbi wa Mlimani City, Jijini Dar es Salaam,  25 Novemba, 2023.

 

“Wakati mwingine tukishafanya maamuzi, kisha tukienda mtaani kuwauliza wanaoyatumia maamuzi hayo tunakuta matokeo ni tofauti na ukirudi kuwauliza waliofanya hayo maamuzi wanasema walifanya bila ya kuwa na taarifa  kamili”

amesema Waziri Nape

 

“Wanafanya maamuzi hayo bila ya kutokujua kwasababu kunakosekana ushirikiano kati ya wafanya maamuzi na wanaoyatumia maamuzi hayo” amesema Waziri Nape

 

Waziri Nape, alisema kuwa vijana wasikae kwenye viti vyao  wakabaki kulaumu, wanachotakiwa ni kufuata utaratibu ili kujua maamuzi yanafanyikaje.

 

Aliongeza kuwa wanatakiwa watumie fursa waliyoipata ili kufuatilia maamuzi yanavyofanyika na kuweza kuchangia maamuzi hayo ili kuwezesha upatikanaji wa maamuzi bora yatakayowasaidia vijana  na  Taifa kwa ujumla.

 

Vilevile,  Waziri Nape amesema kwa sasa Rais Samia ameweza kuifungua Nchi na fursa nyingi zinapatikana na kinachotakiwa  kwa vijana hao kuzitumia fursa hizo vizuri.

 

Katika hatua nyingine Waziri Nape ametumia hafla hiyo kuwashauri vijana kutumia muda wao vizuri katika kujijenga, kuchangia mawazo yenye matokei chanya kwa nchi, kuzitumia vizuri fursa zinazopatikana nchini pamoja kushirikiana katika kujifunza kwa wengine wanaofanya vizuri.