Habari
VIJANA WA KIKE WENYE MAHITAJI MAALUM KUSHIRIKI KIKAMILIFU KATIKA KUIJENGA TANZANIA YA KIDIJITI
DAR ES SALAAM
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye (Mb) amesema kujumuishwa kwa vijana wa kike wa Kitanzania wenye mahitaji maalum katika mafunzo ya TEHAMA kutawasaidia vijana hao kushiriki kikamilifu katika kuijenga Tanzania ya Kidijiti.
Waziri Nape ameyasema hayo wakati wa Hafla ya Kambi Maalum ya Mafunzo kwa Wasichana ya TEHAMA chini ya Muungano wa Wasichana wa Afrika (Tanzania Girls Coding Camp), iliyofanyika tarehe 4 Septemba, 2022 katika ukumbi wa LAPF, Millennium Towers, jijini Dar es Salaam.
“Nimefurahishwa sana na kambi hii ya Connected African Girls; Tanzania Girls Coding Camp inaleta mageuzi katika ujumuishi wa kijiditi kwa kuhakikisha asilimia 15 ya washiriki ni wasichana wasioona na nimeambiwa kuwa wamefanya mambo makubwa ya kushangaza kabisa nawapongeza sana kwa kuwa sehemu muhimu sana.” Amesema Waziri Nape.
Sambamba na hilo Waziri Nape amesema kuwa, mageuzi hayo yanapelekea UNECA kuongeza kipengele cha ujumuishi wa kidijitali kwa kundi la watu wenye mahitaji maalum katika mkakati wake wa mwaka 2023/24.
Naye Mbunge wa Viti Maalum na Mwanzilishi wa OMUKA Hub, Mhe. Neema Lugangira amesema kuwa, Tulichagua vijana wakike ambao hawajawahi kujifunza chochote katika TEHAMA, lakini kama mnavyoona hapa kila kitu wamefanya wenyewe na katika vijana hawa 100 wa kike wapo ambao hawaoni na ambao pia wana ulemavu wa kutokusikia.