Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

UTEKELEZAJI MFUMO WA ANWANI ZA MAKAZI NI ZOEZI ENDELEVU- DKT. YONAZI


Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Jim Yonazi (wa pili kushoto) akikagua nguzo ya jina la Mtaa/barabara wakati wa ziara yake ya ukaguzi wa upatikananji huduma za Mawasiliano na Utekelezaji wa Opersheni Anwani za Makazi katika makazi mapya ya Kijiji cha Msomera kilichopo Kata ya Misima, Wilaya ya Handeni Mkoani Tanga.

HANDENI

Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Jim Yonazi amesema utekelezaji mfumo wa Anwani za Makazi ni zoezi endelevu na halina mwisho kwani wananchi wanajenga na Tanzania inaendelea kukua kilasiku

Dkt. Jim Yonazi ameyasema haya leo tarehe 11 Mei, 2022 wakati wa ziara yake ya ukaguzi wa upatikanaji huduma za Mawasiliano na utekelezaji wa Operesheni Anwani za Makazi katika makazi mapya ya wafugaji na wakulima wa Kijiji cha Msomera kilichopo Kata ya Misima, Wilaya ya Handeni Mkoani Tanga

Amesema kuwa, leo tupo katika Kijiji hiki cha Msomera na tumefurahi kwamba nyumba zimewekewa namba na tunaendelea kuhakikisha kwamba kila mtu anapata Anwani ya Makazi yake, lakini pia zoezi hili ni endelevu na halina mwisho kwa sababu nchi yetu bado inajengwa na  shughuli mbalimbali za maendeleo zinakua kila uchwao, wananchi wanaendelea kuanzisha makazi mapya na kila mtu itakuwa rahisi kutambulika anapoishi na kuweza kunufaika na maendeleo yatokanayo na mfumo huu

Ameongeza kuwa kutokana na zoezi hili kilamtu atajulikana kwa maana sasa ana fursa ya kushiriki katika uchumi wa eneo lake, uchumi wa kitaifa na uchumi wa kimataifa wa Dunia nzima kwa mana kwamba anaweza kupata kiurahisi huduma kama za afya, polisi, zimamoto kwa kujulikana anapoishi

Dkt. Jim amesisitiza kuwa Serikali inahakikisha kila mahali panakuwa na Mawasiliano na kuja kwetu hapa sio kufuatilia utekelezaji wa operesheni Anwani za Makazi pekee lakini pia tumekuja kuangalia hali ya Mawasiliano kwa sababu mawasiliano ndiyo msingi wa maendeleo ya uchumi wa kisasa. Hivyo Mawasiliano ya runinga, redio pamoja na mawasiliano ya simu ni muhimu sana ili wananchi watakapokuja hapa waweze kunufaika na maendeleo ya Teknolojia ya Habari.

Kwa upande wake nae Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Sirieli Mchembe ameishukuru Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa kuja Wilaya ya Handeni na kuwaomba wananchi kuwa na amani na fuhari kwasababu  ya utambulisho waliopewa wa Anwani za Makazi katika nyumba zao kwani itasaidia katika suala la ulinzi na usalama, kurahisiha kufikika kwa urahisi pale ambapo kutatokea dharura ya wagonjwa ama majanga ya moto na kufanyika kwa urahisi shughuli za kibiashara hasa biashara mtandao.