Habari
USHUGHULIKIAJI WA MAKOSA YA MTANDAO UNAFANYIKA KWA UMAKINI MKUBWA - MHANDISI MAHUNDI

Mwandishi wetu, WHMTH.
Naibu Waziri wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Maryprisca Mahundi, amesema Serikali kupitia Wizara hiyo inalitambua tatizo lililopo la wizi wa mitandao nchini na inalishughulikia kwa umakini mkubwa.
Mhandisi Maryprisca ametoa kauli hiyo tarehe 27 Mei, 2024, Bungeni jijini Dodoma wakati akiuliza swali la Nyongeza la Mbunge wa Jimbo la Biharamulo Magharibi Mhandisi Ezra Chiwelesa.
Katika swali lake Mhandisi Chiwelesa, alitaka kujua Je Serikali haioni kwamba ili kuboresha mawasiliano na kusaidia watanzania wanaopata dhuluma, baadhi ya majukumu hasa kuzifikia taarifa za wahalifu zingewekwa chini ya Jeshi la Polisi pekee ili mtu anapoibiwa polisi waweze kuzifikia taarifa kwa haraka na kumuhudumia (muathirika) kuliko Polisi waanze kupeleka taarifa TCRA na kusubiri hadi zirudi?
“Ni kweli Wizara inalitambua hilo na inalishughulikia kwa umakini sana. Kwa taarifa tu ni kwamba Tanzania ni nchi ya pili Afrika katika usalama wa kimtandao hii inaonyesha Wizara ipo makini na tunashughulikia haya yote yanayoendelea mitandaoni,” amesema Mhandisi Maryprisca na kuongeza;
“Mheshimiwa Spika, Jeshi la Polisi tumelipa hii kazi kupitia Kitengo chake (Cyber Crime Unit) kwa hiyo siyo kwamba Jeshi la Polisi halishughuliki moja kwa moja. Lakini maboresho tutaendelea kuyafanya kadri ya ushauri mzuri ambao waheshimiwa wabunge mnaendelea kutupatia”.
Awali akijibu swali la msingi la Mbunge wa Jimbo la Gando, Mhe. Omar Musa Salim, aliyetaka kujua serikali haioni haja ya kuhamisha mfumo wa kushughulikia makosa ya mtandao kuwa chini ya udhibiti wa Jeshi la Polisi, Mhandisi Maryprisca amesema suala la ushughulikiaji wa anga ya mtandao (Cyber space) ni mtambuka haliwezi kutekelezwa kwa ufanisi na taasisi moja hivyo ni muhimu taasisi zinazohusika ziendelee kutekeleza usimamizi huo kwa kushirikiana na kwa utaratibu jumuishi.
“Mkakati wa Taifa wa usalama mtandao umeweka malengo na Mpango wa Kimkakati wa nchi kuhakikisha ulinzi na usalama wa Anga yetu ya kimtandao (Cyber Space) ndani ya mkakati huo taasisi zote zinazohusika na ushughulikiaji wa makosa ya kimtandao zimetambuliwa na majukumu yao kuwekwa bayana ili kuwepo utaratibu mzuri wa kushirikiana,” amesema.
Amezitaja taasisi hizo kuwa ni Tanzania Computer Emergency Responce team, Jeshi la Polisi, ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania na vyombo vingine vya Ulinzi na Usalama.