Habari
USHIRIKIANO KATI YA WIZARA YA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI NA HUAWEI WAJADILIWA KWA KINA
Na Mwandishi wetu Shanghai-China.
Wataalamu kutoka Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari pamoja na taasisi zake, wakiongozwa na viongozi wa sekta hiyo, wamekutana na ujumbe wa wataalamu kutoka Huawei ukiongozwa na Andrew Zhang kujadili namna ya kuimarisha ushirikiano katika maendeleo ya teknolojia ya kidijitali.
Katika kikao hicho, kilichofanyika tarehe 17 Julai, 2026 mjini Shanghai, China wataalamu kutoka Kampuni ya Huawei waliwasilisha maeneo mbalimbali ya ushirikiano ambayo kampuni hiyo imekuwa ikiyatekeleza duniani, wakieleza manufaa yake katika kuharakisha mageuzi ya kidijitali. Maeneo hayo yanajumuisha matumizi ya Akili Unde (AI) katika elimu, ujenzi na uboreshaji wa miundombinu ya TEHAMA (ICT Infrastructure), pamoja na maendeleo ya mifumo ya kidijitali inayosaidia utoaji wa huduma.
Aidha, Kampuni ya Huawei ilieleza uwezo wake katika kutoa suluhisho za teknolojia za kisasa ikiwemo Intelligent Auto Solutions, Digital Power, vifaa janja (Smart Devices), na ujenzi wa vituo vya kuhifadhi na kuchakata taarifa (Digital Data Centers).
Pande zote mbili zilisisitiza umuhimu wa kuendeleza ushirikiano huo ili kuchochea ubunifu, kuongeza ufanisi wa huduma za kidijitali na kuunga mkono maendeleo ya uchumi wa kidijitali.
