Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

USAJILI WA MIUNDOMBINU MUHIMU YA TEHAMA KUIMARISHA ULINZI NA USALAMA WA HUDUMA ZA KIDIJITALI


Na Mwandishi Wetu – WMTH, Dar es Salaam

Serikali kupitia Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imeanza usajili wa Miundombinu Muhimu ya TEHAMA kutoka sekta mbalimbali nchini, ikiwa ni hatua ya kuimarisha usalama, ulinzi na uendelevu wa huduma muhimu za kidijitali nchini.

Hayo yameelezwa Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki (mb) wakati akizungumza na Waandishi wa habari katika Mkutano na Waandishi wa Habari uliofanyika  tarehe 19 Agosti, 2026 katika Ukumbi wa Mikutano wa kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es salaam. 

"Zoezi hilo linatekelezwa kwa mujibu wa Sheria ya Makosa ya Mtandao Na. 14 ya mwaka 2015 na Tangazo la Serikali Na. 147 la tarehe 19 Juni 2026, lililobainisha miundombinu inayopaswa kusajiliwa na kupata ulinzi wa kisheria".

Miundombinu hiyo inahusisha mali, vifaa, mifumo ya kompyuta na mitandao ambayo kutofanya kazi kwake kunaweza kusababisha madhara ya kiusalama, kiuchumi na kijamii. Sekta zinazohusika ni pamoja na fedha na benki, afya, maji, nishati, madini, usafirishaji, kilimo, viwanda, elimu, ulinzi na nyinginezo, huku utambuzi huo ukifanywa kwa ushirikiano wa Serikali na wadau kutoka sekta ya umma na binafsi Tanzania Bara na Zanzibar.

Usajili utawezesha kutambua miundombinu hiyo, kutathmini vihatarishi na kuweka mazingira bora ya kuilinda dhidi ya mashambulizi ya mtandao, hitilafu na majanga. 

Aidha, Wizara imeandaa miongozo ya utambuzi na usimamizi, ukaguzi, tathmini ya vihatarishi, uadilifu na uhalisia wa data pamoja na mipango ya urejeshaji wa huduma baada ya majanga, sambamba na mpango wa kutoa elimu kwa umma kuhusu usajili na ulinzi wa miundombinu hiyo.

Vile vile wamiliki na waendeshaji wametakiwa kusajili miundombinu yao kupitia  https://cii.mawasiliano.go.tz/ huku zoezi hilo likitekelezwa kwa kipindi cha miezi sita kuanzia Juni 19 hadi Desemba 19, 2026. Pia, wamiliki wametakiwa kutoa taarifa kwa mamlaka husika ndani ya saa 24 baada ya kubaini changamoto ya kiusalama, huku Wizara ikiweka dawati la msaada kwa ajili ya usajili, uzingatiaji wa matakwa ya usalama na usaidizi wa kiufundi.

Kwa upande Mwingine Serikali kupitia Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imeonya kuwa uharibifu wa Miundombinu Muhimu ya TEHAMA ni kosa kwa mujibu wa Sheria ya Makosa ya Mtandao, ambapo mhusika anaweza kutozwa faini isiyopungua Shilingi milioni 100 au mara tatu ya hasara iliyosababishwa, au kifungo kisichopungua miaka mitano, au adhabu zote kwa pamoja. 

Wizara imetoa wito kwa taasisi, wadau na wananchi kushirikiana katika kulinda miundombinu hiyo, huku wananchi wakihimizwa kuwa walinzi na mabalozi wa TEHAMA kwa kutumia teknolojia kwa usalama na uwajibikaji.