Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

ULINZI WA FARAGHA ZA WANANCHI KULINDWA KISHERIA


Na Mwandishi Wetu, WMTH – Dodoma

Wadau kutoka Taasisi mbalimbali za Serikali na Sekta Binafsi wamekutana leo Aprili 29, 2025 katika ukumbi wa PSSSF jijini Dodoma kushiriki kikao cha kupokea maoni kuhusu rasimu ya Kanuni za Ada za Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi ya mwaka 2025.

Akizungumza wakati wa kufungua kikao hicho, Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Bi. Salome Kessy, alisema kuwa kanuni hizo zitasaidia kuimarisha ulinzi wa faragha za wananchi — haki ambayo ni ya kikatiba. Aliongeza kuwa utekelezaji wa sheria hii unakwenda sambamba na maono ya 4R za Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Bi. Kessy aliwataka washiriki wa kikao hicho kushiriki kikamilifu kwa weledi ili kutoa maoni yenye mchango chanya katika kuimarisha kanuni hizo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Huduma za Sheria katika Wizara hiyo, Bw. Haruni Matagane, alieleza kuwa lengo kuu la Sheria hiyo ni kuhakikisha taarifa binafsi za wananchi zinapotumika na taasisi yoyote, zifanywe hivyo kwa kuzingatia masharti ya sheria.

Aidha, Mkurugenzi wa Usajili na Uzingatiaji kutoka Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC) Mhandisi Stephen Wangwe, alisema Sheria hiyo inalenga kulinda faragha za wananchi kwa kuzuia matumizi holela ya taarifa zao, akitolea mfano wa watu kupigwa picha au video katika hafla kama harusi au misiba bila ridhaa yao na picha hizo kusambazwa mitandaoni.

Naye Mkurugenzi wa Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi Ofisi ya Zanzibar, Bi. Rehema Abdallah, alisema uwepo wa Sheria hiyo utaziwezesha Taasisi za Zanzibar kushiriki kikamilifu katika kulinda faragha za wananchi, pamoja na kupanua wigo wa usimamizi wa taarifa binafsi. Alisema kuwa hii itaongeza imani hususan kwa watumiaji wa huduma za kidijitali kutokana na uhakika wa Ulinzi wa Taarifa na faragha zao.