Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

UJENZI WA MIFUMO YA TEHAMA KUBORESHA UFANISI NA KUKUZA UCHUMI WA KIDIJITALI


Na Mwandishi Wetu, WMTH, Arusha.

Wizara ya  Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imefanikisha ujenzi wa mifumo mitano ya TEHAMA kwa mwaka wa fedha 2024/25 itakayoongeza ufanisi wa sekta za umma na binafsi na kukuza Uchumi wa kidijitali.

Mifumo hiyo ni pamoja na Mfumo wa Ubadilishanaji Taarifa (Jamii X-change na ZanXchange), Mfumo wa utambuzi kidijitali (Jamii Namba) mfumo wa Utambuzi wa wateja (e-KYC), Mfumo wa malipo ya kidijitali Jamii Pay na mfumo wa usajili na uwezeshaji wa Wadau wa ikolojia ya tafiti na bunifu za TEHAMA ikiwemo kampuni changa (safari hunt);

Hayo yamezungumzwa na Mhe. Mhandisi Maryprisca Winfried Mahundi (Mb), Naibu Waziri Wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari wakati akihutubia kwenye hafla ya Ufunguzi wa Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi la Wizara hiyo lililofanyika Februari 18, 2025 katika ukumbi wa mikutano wa Jengo la PAPU mkoani Arusha.

Aidha, Mhandisi Mahundi amelitaka Baraza hilo kuhakikisha linawezesha ushiriki wa Wafanyakazi wote katika utekelezaji wa shughuli za Wizara na kusimamia kwa ufanisi utekelezaji wa Sera, Sheria, Kanuni,Taratibu na Miongozo inayohusu haki, wajibu na stahili za Wafanyakazi pamoja na Utawala Bora. 

“Ninatoa wito kwa Menejimenti kuwa na uhusiano mzuri na Watumishi na kuhakikisha kuwa haki na stahili za Watumishi zinatolewa kwa wakati”, amesisitiza Mhandisi Mahundi.

Naye Katibu Mkuu na Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara hiyo, Bw. Mohammed Khamis Abdulla amewataka watumishi wa Wizara hiyo kuwa wazalendo na kufanya kazi kwa kujituma na kwa bidii, kwani hakuna haki bila wajibu hivyo wanapaswa kuwajibika ndipo wadai haki zao.

Naye, Mwenyekiti wa TUGHE Tawi la Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Bi. Laurencia Masigo amesema Baraza hilo ni chombo cha kuboresha mahusiano, umoja na ushirikishwaji wa watumishi ili kuongeza ufanisi mahali pa kazi pamoja na maslahi ya watumishi yanayoenda sambamba na uwajibikaji wao.