Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

UHURU WA VYOMBO VYA HABARI UNATOKANA NA UTASHI WA KISIASA - WAZIRI NAPE


Na Mwandishi Wetu - WHMTH

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Moses Nnauye (Mb) amesema uhuru wa vyombo vya habari unaoshuhudiwa sasa unatokana na utashi wa Kisiasa wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na wasaidizi wake.

Waziri Nape alisema hayo Aprili 03, 2024 wakati wa maadhimisho ya Kilele cha Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani, yaliyofanyika kitaifa jijini Dodoma na kusisitiza kuwa hali ya uhuru wa vyombo vya habari nchini inaendelea kuimarika. 

"Hatujafika tunakotaka kwenda lakini kwa hakika hatupo tulipokuwa jana. Mazingira ya jana na leo ni tofauti na wanahabari wanakubaliana na mimi. Tumefika hapa kwenye maboresho haya yaliyofanyika kwa sababu ya utashi wa kisiasa wa Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan", alisisitiza.

Waziri Nape alisema Serikali imekuwa ikihakikisha inasimamia uhuru huo kwa kutekeleza R4 za Mhe. Samia kuhakikisha sekta hiyo inaimarika na kunakuwa na utulivu uliopo na wengi wameshuhudia na kutoa mifano kadhaa ya hatua ambazo zimechukuliwa.

"Mara kadhaa yeye (Rais Samia) na ninyi wasaidizi wake (Waziri Mkuu) mmekuwa mkitushauri kwamba tuendelee kuwa walezi na wasimamizi wa sekta hii kuwapa uhuru zaidi kadri muda unavyoenda. Na ushahidi upo, tumechukua hatua kadhaa mojawapo ikiwa ni marekebisho ya sheria na katika hili niseme tulipofanya mapitio ya sheria baadhi ya mambo yaliyokuwepo kwenye sheria yana msingi wake kwenye sera," alisema.

Waziri Nape alisisitiza kwamba kwa sababu Serikali inapitia sera iliyopo ahadi yake kwa wanahabari, ni kwamba mapitio ya sera yatakapokamilika baadhi ya mambo ambayo hayakuwezekana kubadilishwa yatafanyiwa mabadiliko kwenye sheria.

Aliwataka wanahabari kuwa wavumilivu wakati Serikali inashughulikia mabadiliko hayo ya sera ili yaende sanjari na Sheria.

"Huwezi kwenda kubadilisha sheria wakati sera ina msimamo huo. Ndiyo maana tukasema, badala ya kusubiri mabadiliko ya sera, Rais Samia akasema kwa kuwa sheria inapigiwa kelele sana fanyeni mabadiliko ya sheria yale yanayohitaji mabadiliko ya sera yatasubiri. Nataka nikuhakikishieni nia ya Rais Samia ni kuhakikisha tunapata uhuru kamili wa vyombo vya habari. Na huko ndiko tunakokwenda tuvumiliane, tukamilishe sera", alisema Waziri Nape.