Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

UFUNGUZI WA MAFUNZO YA UHAKIKI WA TAARIFA ZA ANWANI ZA MAKAZI  KWA WENYEVITI WA SERIKALI ZA MTAA NA WATENDAJI WA KATA NA MITAA KATIKA HALMASHAURI YA MANISPAA YA UBUNGO – DAR ES SALAAM.


Na. Simon Kibarabara

Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam Ndg. Saloni Nyika , leo Juni 19, 2023 amefungua mafunzo ya siku tatu ya kujenga uwezo kwa Wenyeviti wa Serikali za Mitaa na Watendaji wa Kata na Mitaa kuhusu utekelezaji wa zoezi la uhakiki wa taarifa za Anwani za Makazi ndani ya Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo.

Akifungua mafunzo hayo yaliyofanyika katika Ukumbi wa La Dariot, Kaimu Katibu Tawala ametumia nafasi hiyo kuwataka Wenyeviti na watendaji wa Mitaa kushirikiana na wajumbe wa Serikali za Mitaa pamoja na wananchi kwa ujumla ili kuhakikisha kazi ya kuhakiki taarifa za Anwani za Makazi inafanikiwa na kuleta tija iliyokusudiwa. 
“Wenyeviti wa serikali za mitaa, niwaombe mkashirikiane na wajumbe wenu kuhamasisha wananchi kutoa ushirikiano katika utekelezaji wa zoezi la Uhakiki wa Taarifa za Anwani za Makazi” alisema Bw. Nyika.

Aidha, Ndg. Nyika pamoja na masuala mengine, alisisitiza utunzaji na ulinzi shirikishi wa Miundombinu ya Mfumo wa Anwani za Makazi ambayo aliitaji kuwa nguzo za majina ya barabara na vibao vya namba za nyumba. 

Kwa upande wake Ndgu Mulembwa Munaku, Mkurugenzi wa Huduma za Mawasiliano wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari amesema kwamba Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imedhamilia kuimarisha shughuli za utambuzi nchini ili kuchochea kasi ya ukuaji wa uchumi hususan uchumi wa kidijitali. 

Kazi ya kujenga uwezo kwa Wenyeviti wa Serikali za Mitaa na Watendaji wa Kata na Mitaa ni Mpango endelevu wa Serikali unaolenga kujenga mazingira ya utekelezaji endelevu wa Mfumo wa Anwanzi za Makazi nchini.