Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

UELEWA MDOGO KATIKA MATUMIZI YA VIFAA VYA TEHAMA KUCHOCHEA UHALIFU MTANDAONI : MHANDISI KUNDO  


Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliiano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Mhandisi Kundo Mathew (Mb) ameeleza kuwa kuwepo kwa uelewa mdogo kwa watumiaji wa vifaa vya TEHAMA huchangia uhalifu mtandaoni.
 
Ameeyasema hayo wakati akifungua Kongamano la Maadhimisho ya Siku ya Usalama mtandaoni lililofanyika leo 07 Februari, 2023, katika ukumbi wa PSSSF, jijini Dodoma.
 
“Imebainika kuwa watumiaji kwa kiasi kikubwa ndiyo wanaochangia kufanikisha matukio mengi ya kiusalama. Hii ni kutokana na uelewa mdogo wa matumizi sahihi ya TEHAMA au kutozingatia kanuni za kiusalama (Security Best Practices)”. Amesema Mhe. Kundo

Aidha, Mhe Kundo ameeleza umuhimu wa kuendelea kutoa elimu ya matumizi sahihi na salama ya TEHAMA na mtandao ili kuepuka athari za kiusalama.
 
Katika hatua nyingine, Naibu Waziri kundo ameipongeza Wizara ya Habari, Mawasiliiano na Teknolojia ya Habari pamoja na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kwa kazi nzuri inayofanyika ya kuhakikisha Tanzania inakuwa na mtandao salama.
 
“Naomba nitumie nafasi hii kuipongeza Wizara na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kwa kazi nzuri inayofanyika ya kuhakikisha tunakuwa na mtandao salama.” Amesema Mhandisi Kundo