Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

UCSAF YATAKIWA KUDHIBITI MFUMO WA TARATIBU ZA MANUNUZI NA USAMBAZAJI WA VIFAA VYA TEHAMA MASHULENI


 KYERWA

Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Mhandisi Kundo Mathew ameitaka taasisi ya mawasiliano ya Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) kuimarisha na kusimamia ipasavyo taratibu za manunuzi na usambazaji wa vifaa vya TEHAMA mashuleni ili kuhakikisha kinachotarajiwa kufika katika shule husika kinafika bila mapungufu yeyote.

Mhandisi Kundo ameyasema hayo alipotembelea Shule ya Sekondari Mabira iliyopo katika Wilaya ya Kyerwa Mkoani Kagera kwa ajili ya kukagua chumba cha kompyuta cha shule hiyo kilichowezeshwa vifaa vya TEHAMA na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na kukuta kuna vifaa vingine vya TEHAMA vilivyopelekwa katika shule hiyo kwa ufadhili wa UCSAF

Hata hivyo baada ya kukagua idadi ya kompyuta zilizopelekwa na UCSAF katika shule hiyo zilionekana zipo kompyuta nne na printa moja ambapo ndio idadi aliyothibitisha kupokea Mkuu wa Shule hiyo aliyefahamika kwa jina la Danford Nuvia

Aidha, ilifahamika kuwa idadi hiyo ni pungufu kulingana na utaratibu wa Mfuko huo wa kupeleka kompyuta tano na printa moja katika miradi yake ya kusambaza vifaa vya TEHAMA katika shule za msingi na sekondari nchini

“Sitaki kufumbia macho mapungufu, tukifumbia macho tutajikuta Serikali inatumia fedha nyingi kwa ajili ya vijana wetu halafu kunakuwa na ujanja ujanja, iwapo kila shule ikipelea kompyuta moja maana yake ni kuna watu wanaingiza mfukoni wanapeleka sehemu nyingine”, alizungumza Mhandisi Kundo

Mhandisi Kundo alitoa maelekezo kwa Mfuko huo kupitia kwa Mkuu wa Uendeshaji wa UCSAF alieambatana nae katika ziara hiyo kuhakikisha wanaboresha Mfumo mzima wa taratibu za manunuzi na usambazaji ili kujiridhisha kuwa kilichotakiwa kufika kimefika kama kilivyokusudiwa

“Tusipokuwa makini kwenye usambazaji maana yake ni kujikuta misaada hii haifiki kwa walengwa wakati nyaraka zetu za ofisini tunaandika tumeshamaliza kupeleka vifaa vya idadi fulani kwenye shule fulani kumbe tunakuwa tunadanganya watu”, aliongeza Mhandisi Kundo

Sambamba na hilo alitoa wito kwa wakuu wa shule baada ya kupokea vifaa vya TEHAMA kutoka katika Mfuko huo au wafadhili wengine kuhakikisha wanawasiliana nao ili kuthibitisha kile walichopokea kutoka kwa msambazaji ndicho kilichokusudiwa kufika

Chumba cha Kompyuta cha Shule ya sekondari Mabira kimefadhiliwa vifaa vya TEHAMA na TCRA ambapo kwa mujibu wa Mkuu wa TCRA Kanda ya Ziwa Mhandisi Francis Mihayo  amesema vifaa hivyo vimegharimu kiasi cha shilingi Milioni 49.7 ambavyo ni kompyuta 10, printa kwa ajili ya maandishi ya nukta nundu 1, Kiambo yaani LAN ( Local Area Network)  na Mtandao wenye kasi ya 2mbps iliyolipiwa kwa mwaka mzima.