Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

UCSAF YAKABIDHI VIFAA VYA TEHAMA SHULE YA SEKONDARI DUTWA NA NKOLOLO ZILIZOPO WILAYA YA BARIADI


Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhandisi Kundo Mathew (wa pili kulia) akikabidhiwa kompyuta na Mkuu wa Uendeshaji wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) (aliyevaa barakoa) wa kwanza ni Mkuu wa Wilaya ya ya Bariadi Mhe. Lupakisyo Kapange

 

SIMIYU

Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) imekabidhi vifaa vya TEHAMA kwa ajili ya Shule ya Sekondari Dutwa na Shule ya Sekondari Nkololo zilizopo katika Wilaya ya Bariadi ambavyo ni kompyuta 10 na printa 2 ambapo kila shule imepatiwa kompyuta 5 na pinta 1

Vifaa hivyo vimekabidhiwa kwa Mbunge wa Bariadi ambaye pia ni Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhandisi Kundo Mathew ambaye ndiye aliyevikabidhi katika shule hizo akiambatana na Mkuu wa Wilaya hiyo Mhe. Lupakisyo Kapange

“TEHAMA inaenda kuchangia kukuza uchumi wa dunia na sisi Tanzania tumeona kwamba tusibaki nyuma katika kukuza matumizi ya TEHAMA kwa kuhakikisha vijana wetu wanajifunza TEHAMA kuanzia shuleni na nikiwa kama Mbunge wa Bariadi nina kila sababu ya kuwasisitiza vijana wetu kusoma kwa bidii”, amezungumza Mhandisi Kundo

Naibu Waziri huyo ametoa rai kwa wanafunzi hao kusoma kwa bidii ili kupata ufaulu mzuri katika mitihani yao ya Kitaifa na kusisitiza kuwa wanafunzi watakaopata ufaulu wa daraja la kwanza la pointi 7,8,9 atawalipia ada kama alivyoahidi wakati wa kampeni ya uchaguzi mwaka 2020

Ameongeza kuwa mpaka sasa amekwishawalipia ada wanafunzi 18 wa kidato cha tano ambao wamepata ufaulu huo katika matokeo ya mwaka huu na wale ambao wamefaulu lakini familia zao zimethibitishwa kuwa hazina uwezo wa kuwaendeleza

Kwa Upande wa Mkuu wa Uendeshaji wa UCSAF Eng. Albert Richard amesema moja ya majukumu yanayotekelezwa na Mfuko huo ni kupeleka vifaa vya TEHAMA katika shule za umma ili kuendelea kuinua matumizi ya TEHAMA nchini

Naye Mwalimu Mekrina Bonifasi wa Shule ya Sekondari Dutwa amesema kuwa msaada huo wa kompyuta utakuwa chachu ya ufaulu na utasaidia sana katika ufundishaji na ujifunzaji kwa wanafunzi hasa ukizingatia kuwa kwa sasa shule hiyo ina wanafunzi wa kidato cha kwanza wapatao 280 ambao wanasoma somo la kompyuta na watafanya mtihani wa Taifa 2022 kwa mara ya kwanza

Katika hatua nyingine Naibu Waziri huyo ambaye pia ndiye Mbunge wa Bariadi amesikitishwa na uongozi mzima wa Kata ya Nkololo kwa kushindwa kusimamia ujenzi wa maabara ya TEHAMA katika shule ya Sekondari Nkololo wakati tayari Mbunge huyo alikwishapeleka mifuko 156 ya simenti na mabati 50 toka mwezi Machi, 2020 lakini mpaka sasa hakuna chochote kilichofanyika zaidi ya kufyatua tofali 1500

Ameongeza kuwa, mwaka 2025 Chama Cha Mapinduzi (CCM) kitakuja kuulizwa kimetekeleza nini wakati jitihada zinafanyika za kuleta nyenzo za kutekeleza yale ambayo yameandikwa kwenye Ilani ya Chama hicho ambayo ndani yake imeongelea masuala ya TEHAMA lakini bado viongozi wa Chama na Serikali katika ngazi ya Kata hiyo wameshindwa kusimamia utekelezaji wa yale yaliyokusudiwa

Naye Mkuu wa Wilaya hiyo Mhe. Lupakisyo Kapange amemuelekeza Mkurugenzi wa Halmashauri na Wataalam wake wahakikishe wanatoka ofisini na kwenda kuweka kambi katika shule hiyo ili kusimamia ujenzi wa darasa hilo hadi ukamilike

“Baada ya hapa nataka nipate maelezo kwanini darasa halijakamilika kutoka mwezi Machi mpaka sasa na wakati vifaa vyote vipo, nani alikuwa anasimamia, nani alipinga na nani alichelewesha na taarifa hiyo niipate ndani ya wiki moja” alizungumza Mhe. Kapange

Aidha, iliamuliwa kuwa vifaa vya TEHAMA vilivyopelekwa kwa ajili ya Shule ya Sekondari Nkololo vihifadhiwe na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Bariadi mpaka hapo chumba cha maabara ya TEHAMA ya shule hiyo kitakapokamilika ndio