Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

MAGEUZI YA KIDIJITALI YAPEWA KIPAUMBELE BAJETI YA 2026/2027


Na Mwandishi Wetu, WMTH, Dodoma.

 

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki (Mb) amesema Serikali imeipa kipaumbele ajenda ya mageuzi ya kidijitali katika Bajeti ya mwaka 2026/2027 kwa lengo la kuongeza ukusanyaji wa mapato, kupanua wigo wa kodi na kuimarisha uwazi wa kifedha kupitia matumizi ya teknolojia za kisasa ikiwemo Akili Unde (AI), Big Data na Blockchain.

 

Akichangia makadirio ya mapato na matumizi ya Hotuba ya Serikali Juni 22, 2026 Bungeni jijini Dodoma, Waziri Kairuki amesema mfumo wa kidijitali wa mapato unaojengwa utaimarisha ukusanyaji wa kodi kupitia malipo ya kidijitali, mashine za EFD, Jamii Namba na mifumo mingine ya kisasa, huku ukisaidia kurasimisha sekta isiyo rasmi na kuongeza ushiriki wa wananchi katika uchumi rasmi.

 

Waziri Kairuki amebainisha kuwa kwa mara ya kwanza bajeti kuu ya Serikali imeweka msisitizo mkubwa katika mageuzi ya kidijitali, jambo linalodhihirisha kuwa TEHAMA imehama kutoka kuwa sekta saidizi na sasa imekuwa injini kuu ya utekelezaji wa malengo ya maendeleo ya kiuchumi na kifedha ya  Taifa.

 

Ameongeza kuwa, Serikali inaendelea kuhamasisha matumizi ya Lipa Namba na TanQR pamoja na kutekeleza mapendekezo ya Tume ya Rais ya Maboresho ya Kodi, ikiwemo kuunganisha mifumo mbalimbali ya Serikali na kutumia Akili Unde, Big Data na Blockchain ili kuongeza ufanisi, kupunguza urasimu na kuziba mianya ya upotevu wa mapato.

 

Katika kuimarisha miundombinu ya mawasiliano, Waziri Kairuki amesema Serikali itaendelea kukamilisha ujenzi wa kilometa 186 za Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano kuelekea Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), kuunganisha wilaya 17 na kukamilisha uunganishaji wa mifumo takribani 110 ya TEHAMA. Aidha, Serikali imekamilisha mfumo wa malipo wa Jamii Pay ulioboreshwa na inaendelea na juhudi za kurahisisha malipo ya kidijitali kupitia mfumo wa TIPS.

 

Waziri Kairuki ameeleza kuwa, Serikali inaandaa Mkakati wa Taifa wa Akili Unde na inaendelea kujenga Mfumo wa Kitaifa wa Modeli Kubwa ya Lugha ya Kiswahili ambao utasaidia maendeleo ya mifumo ya Akili Unde inayotumia Kiswahili kwa ufasaha, usahihi na kwa kuzingatia mazingira ya Tanzania.