Habari
Serikali Yaongeza Nguvu kwa Polisi Zanzibar Kupambana na Uhalifu wa Kimtandao
Serikali kupitia Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imeeleza kuwa itaendelea kuimarisha uwezo wa Jeshi la Polisi kwa kuwekeza katika miundombinu ya TEHAMA, vifaa vya kisasa na mafunzo ya kitaalamu ili kukabiliana na ongezeko la uhalifu wa kimtandao unaoambatana na maendeleo ya teknolojia duniani.
Akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi vifaa vya uchunguzi wa kidijitali kwa Makao Makuu ya Polisi Zanzibar, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Bw. Mohammed Khamis Abdulla, amesema kuwa Serikali inalenga kuhakikisha usalama wa wananchi, mali zao na mifumo ya kidijitali inayotumika katika shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi inakuwa na manufaa makubwa katika kukuza uchumi na kuboresha utoaji wa huduma nchini.
Amefafanua kuwa wahalifu wameanza kutumia teknolojia za kisasa ikiwemo Akili Unde (AI) kufanya vitendo vya udanganyifu, kuunda sauti, picha na video bandia (deepfakes), pamoja na kusambaza taarifa za uongo zinazoweza kupotosha umma na kuhatarisha usalama wa jamii. Kutokana na hali hiyo, Serikali imejipanga kuhakikisha vyombo vya usalama vinakuwa na uwezo wa kutambua, kuchunguza na kuchukua hatua dhidi ya wahalifu hao kwa mujibu wa sheria za nchi.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Bw. Ally Senga Gugu, ameipongeza Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa mchango wake katika kuimarisha uwezo wa Jeshi la Polisi Zanzibar. Huku akiongeza kuwa ushirikiano huo unasaidia kuongeza ufanisi wa vyombo vya usalama katika kulinda wananchi, mali zao na kuhakikisha matumizi ya teknolojia yanafanyika kwa usalama.
Bw. Abdulla amesema vifaa vilivyokabidhiwa vitasaidia kuongeza ufanisi kwa viwango vinavyokubalika kitaifa na kimataifa na kusisitiza kuwa pamoja na uwepo wa vifaa vya kisasa, maendeleo ya teknolojia yanahitaji uwekezaji endelevu katika rasilimali watu ili wataalamu wa uchunguzi wa kidijitali waweze kuendana na mabadiliko ya teknolojia duniani.
Vilevile, ameongeza kuwa Wizara itaendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi pamoja na taasisi nyingine za Serikali katika kuimarisha usalama wa taarifa, kujenga uwezo wa wataalamu na kuhakikisha mazingira salama ya matumizi ya teknolojia yanachangia kukuza uchumi wa kidijitali na maendeleo endelevu nchini.
