Habari
Serikali Yaimarisha Fursa za Kidijitali kwa Maendeleo ya Wananchi
Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imeendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu fursa za TEHAMA wakati wa Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea Chinangali Park, Dodoma.
Akizungumza kupitia kipindi cha redio A FM, Afisa TEHAMA Mkuu, Bw. Nkinde Moses, alisema Serikali inaendelea kuimarisha miundombinu na huduma za kidijitali ili kurahisisha upatikanaji wa huduma na kuongeza ushiriki wa wananchi katika uchumi wa kidijitali.
Alieleza kuwa vijana wanaweza kutumia majukwaa ya kidijitali kupata mafunzo, kujiendeleza kitaaluma na kutangaza bidhaa, huduma na ubunifu wao ili kuvutia wawekezaji na wadau wa maendeleo.
Kwa upande wake, Afisa Mawasiliano wa TCRA, Bi. Herieth Shija, alisema takwimu za Machi 2026 zinaonesha usajili wa huduma za intaneti nchini umefikia milioni 58.9, ishara ya kuongezeka kwa matumizi ya teknolojia na fursa zake za maendeleo.
Wataalamu hao pia walikumbusha wananchi, hususan vijana, kutumia teknolojia kwa usalama na kuepuka uhalifu wa mtandaoni, huku kampeni za elimu kuhusu usalama wa kidijitali zikiendelea kutolewa kwa umma.
