Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

Tuutumie mfumo wa Anwani za Makazi NaPA- DED Mbarali


Na Mwandishi Wetu, WHMTH Dar es Salaam

Wito umetolewa kwa Watanzania kutumda Mfumo wa Anwani ya Makazi, kupitia Programu Tumizi kwa umma (NaPA), kwani unasaidia kurahisisha mawasiliano na kupata taarifa kwa urahisi na bila usumbufu wowote.

Wito huo umetolewa tarehe 06 Julai, 2024 na Mkurugenzi Mtendaji (DED) wa Halmashauri ya Mbarali, mkoani Mbeya, Bw. Missana Kwangura, alipotembelea Banda la Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, katika Maonesho ya 48 ya Kimataifa ya Biashara, katika Viwanja vya Maonesho vya Julius Nyerere, Barabara ya Kilwa, mkoani Dar es Salaam.

Bw. Kwangura amesema akiwa katika banda hilo pamoja na mambo mengine, amejifunza kutumia Anwani ya Makazi kwa kutumia mfumo wa NaPA aliosema una vitu vingi vya kusaidia kurahisisha mawasiliano na kuweza kufika popote, hivyo ni vizuri kila mtu akatumia mfumo huo.

"Mfumo huu una vitu vingi, kama unataka mahoteli, kama unataka huduma za kibenki, kama unataka nyumba za watu, kwa sababu vitu vingi vimewekwa kwenye mfumo, hivyo unatusaidia kurahisisha mawasiliano, lakini pia unatusaidia kutokuuliza sana, kwa sababu unaweza kuuliza, mtu mwingine akakueleza tofauti", alisema Kwangura.

Alisema, matumizi ya mfumo huo ni rahisi, kwani ni suala dogo la kuingia kwenye mfumo wa NaPA, baada ya hapo unaweza kwenda unapotaka bila changamoto yoyote au matatizo yoyote.

Bw. Kwangura aliyeambatana na Afisa Biashara wa Halmashauri hiyo Bw. John J. Luena amesema Elimu waliyoipata kuhusu Mradi wa Tanzania ya Kidigitali pamoja na Mfumo wa Anwani za Makazi (NaPA) imewasaidia na watakwenda kuitumia vizuri katika Halmashauri yao.

Katika maelezo yake mmoja wa Maafisa kutoka Wizara hiyo Bw. Innocent Jacob amesema NaPA ni mfumo wenye taarifa zinazosaidia katika uandaaji wa Mipango mbalimbali ya maendeleo ndani ya Halmashauri endapo utatumika kikamilifu.