Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

Naibu Waziri Mahundi : Msitoe taarifa binafsi mitandaoni


Na Mwandishi Wetu, WHMTH, Mbeya

Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhandisi Maryprisca Mahundi (Mb) amewataka watanzania kuacha kutoa taarifa zao binafsi kwenye mitandao ya kijamii kwani dunia imeharibika.

Amesema wao viongozi kwa nafasi zao wanaendelea kutekeleza wajibu wa kuhakikisha wanadhibiti tabia hizo zinazofanyika katika maeneo mbalimbali hapa nchini.

Mhandisi Mahundi amesema hayo Julai 12, 2024 wakati akizungumza na wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Katoliki Mbeya (CUCoM).

"Huko mnako cheza cheza kwenye mitandao ya kijamii msiweke taarifa zenu binafsi na msipende kuandika ovyo mfano Facebook, Twitter, Instagram na mitandao mingine ya kijamii Dunia imeharibika hivi Sasa umakini ni muhimu "amesema Mhandisi Mahundi na kuongeza;

"Mimi na wewe lazima tudhibiti pamoja tunza taarifa zako usimpe mtu yeyote na usimwamini mtu leo mpo kwenye urafiki kesho mkikosana amezipeleka halafu inakuja kuleta shida," amesema Mhandisi Mahundi.

Aidha Mhandisi Mahundi amesema katika kuhakikisha inatekeleza kwa vitendo jukumu lake miezi miwili iliyopita Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, ilizindua Tume ya kutunza taarifa za mtu binafsi.

Hata hivyo amesema bado wapo watu watukutu mtaani wanaokopesha fedha ndogo ndogo kuanzia sh.100,000 kushuka chini na mtu akichelewa kulipa zinatumwa jumbe za vitisho kwa watu waliopo kwenye simu ya mkopaji.

"Pametokea ombwe kubwa sana mitaani la kukopesha ...mkopaji akichelewa tu wale watu waliopo kwenye simu ya mkopaji wanaanza kutumiwa sms za vitisho kuwa bwana David alikopa kiasi fulani cha fedha na kuwa wewe ni mmoja wa wadhamini wake sababu tu mnawasiliana mara kwa mara na wakati huo David anakopa hakukuwa na mawasiliano yeyote na hivyo mwisho wa siku unakuta unapigwa picha bila kujijua," amesema Mhandisi Mahundi.

Amesisitiza Mhandisi Mahundi ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Mbeya pia amesema kwamba Wizara inashirikiana na Jeshi la Polisi kupitia Kitengo cha "Cyber" kushughulikia changamoto hiyo kwa kutoa matangazo kwa wananchi kuwa makini na taarifa zao binafsi.

Baadhi ya wanachuo walioshiriki mkutano huo wamesema kuwa mitandao ya kijamii imekuwa changamoto kubwa na baadhi ya vitendo vya udhalilishaji vimekuwa vikipitia huko .