Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

TANZANIA NA ITU KUIMARISHA USHIRIKIANO WA KUHARAKISHA MAGEUZI YA KIDIJITALI


Na Mwandishi wetu Geneva, Uswisi.

 

Tanzania imeahidi kuendelea kuimarisha ushirikiano na Shirika la Kimataifa la Mawasiliano Duniani (ITU) ili kuharakisha mageuzi ya kidijitali kupitia upanuzi wa huduma za mawasiliano, kuimarisha usalama wa mtandao, kukuza ujumuishaji wa kidijitali na kuongeza matumizi ya teknolojia zinazoibuka.

 

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki (Mb) alipokutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi wa Ofisi ya Maendeleo ya Mawasiliano ya ITU (BDT), Dkt. Cosmas Zavazava, katika kikao kilichofanyika jijini Geneva.

 

Mhe. Kairuki ameeleza kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana kwa karibu na ITU katika kutekeleza ajenda ya mageuzi ya kidijitali kupitia upanuzi wa huduma za intaneti ya kasi, kuongeza ujuzi wa kidijitali, matumizi ya Akili Unde (AI), kuimarisha usalama wa mtandao, kuendeleza huduma za serikali mtandao na mifumo ya tahadhari za mapema.

 

Vilevile, Mhe Kairuki amebainisha kuwa Tanzania imeendelea kupata mafanikio makubwa katika sekta ya TEHAMA, ikiwemo kuboresha nafasi yake katika Kielelezo cha Kimataifa cha Usalama wa Mtandao (Global Cybersecurity Index), kushiriki katika utekelezaji wa Kielelezo cha Maendeleo ya TEHAMA (ICT Development Index), pamoja na kuendelea kuwekeza katika upanuzi wa huduma za intaneti vijijini na mijini kupitia Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano.

 

Kwa upande wake, Dkt. Zavazava aliipongeza Tanzania kwa dhamira yake ya kuharakisha mageuzi ya kidijitali na kueleza kuwa ITU itaendelea kuisaidia nchi kupitia utoaji wa utaalamu, kujenga uwezo wa wataalamu na kusaidia upatikanaji wa rasilimali kwa ajili ya utekelezaji wa vipaumbele vya maendeleo ya kidijitali.

 

Vilevile, aliongeza kuwa baadhi ya programu zinazotekelezwa na Shirika hilo ni pamoja na vituo vya mageuzi ya kidijitali (ITU Academy, Digital Transformation Centres) na mtandao wa vituo 17 vya Kuharakisha Ubunifu katika Teknolojia za Kidijitali (Digital Innovation Acceleration Centres), vinavyosaidia nchi wanachama kujenga ujuzi wa kidijitali, kuhamasisha ubunifu na kukuza uchumi wa kidijitali.

 

Dkt. Zavazava pia aliwasilisha mfumo wa serikali mtandao unaotumia Akili Unde na programu huria (open-source), akieleza kuwa unaweza kupunguza kwa kiwango kikubwa gharama za utoaji wa huduma za kidijitali za serikali ikilinganishwa na mifumo ya kibiashara.

 

Aidha, alisema ITU inaendelea kuandaa na kusambaza zana za kisasa za upangaji zitakazosaidia nchi kubaini teknolojia bora za kupanua miundombinu ya kidijitali, pamoja na kutathmini athari za kijamii na kiuchumi za uwekezaji katika sekta ya mawasiliano kabla ya utekelezaji wa miradi.

 

Akizungumzia ujumuishaji wa kidijitali, Dkt. Zavazava alisisitiza umuhimu wa kuwawezesha wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kupata ujuzi wa kidijitali na kushiriki kikamilifu katika masuala ya usalama wa mtandao, ubunifu wa teknolojia na biashara mtandao.

 

Naye Mhe. Kairuki aliishukuru ITU kwa ushirikiano wake wa muda mrefu na kueleza kuwa Tanzania ina nia ya kuwa mwenyeji wa vituo vya kikanda vya mafunzo ya kidijitali na vituo vya umahiri, huku ikiwa tayari kushirikisha mataifa mengine uzoefu wake katika utekelezaji wa miradi ya mageuzi ya kidijitali iliyofanikiwa.