Habari
TANZANIA YATOA WITO WA KUIMARISHWA KWA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA KATIKA UTAWALA WA AKILI UNDE
Na Mwandishi Wetu, Geneva - Uswisi
Serikali ya Tanzania imetoa wito wa kuimarishwa kwa ushirikiano wa kimataifa ili kuhakikisha maendeleo ya kasi ya Akili Unde (AI) yanasimamiwa kupitia mifumo ya kimataifa iliyo jumuishi, yenye uwazi na usawa, ikitahadharisha kuwa nchi zinazoendelea hazipaswi kuachwa nyuma wakati teknolojia hiyo ikiendelea kubadili uchumi na jamii.
Akizungumza mbele ya zaidi ya wajumbe 190 wanaowakilisha serikali, mashirika ya kimataifa, sekta binafsi na jamii ya teknolojia duniani katika Mdahalo wa Kimataifa kuhusu Utawala wa Akili Unde (Global Dialogue on AI Governance), tarehe 6 Julai, 2026, Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah Jasmine Kairuki (Mb), aliwasilisha Dira ya Tanzania ya kutumia Akili Unde kama kichocheo cha maendeleo ya Taifa huku ikiimarisha mifumo ya kuhakikisha matumizi yake yanakuwa ya kuwajibika.
Waziri Kairuki alisema Tanzania inaichukulia Akili Unde kuwa nguzo muhimu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 na kichocheo muhimu cha uchumi wa kidijitali unaochipukia. Alieleza kuwa Serikali inaendelea kutekeleza mageuzi ya kina ya sera na mifumo ya udhibiti ili kuweka mazingira imara yanayochochea ubunifu huku yakilinda haki za wananchi na kujenga imani ya umma.
“Tanzania inaamini kuwa Akili Unde ina uwezo wa kuleta mageuzi katika sekta za kilimo, afya, elimu, huduma za kifedha na utawala wa umma,” alisema Mhe. Kairuki. “Hivyo, matumizi yake yanapaswa kuwa salama, jumuishi na yalenge kuhakikisha wananchi wote wananufaika.”
Alieleza hatua zinazotekelezwa kuimarisha utawala wa Akili Unde, ikiwemo kuandaa mifumo ya udhibiti, kuboresha mifumo ya usimamizi wa data, kuimarisha ulinzi wa faragha na usalama wa mtandao, pamoja na kuandaa miongozo ya kitaifa ya matumizi ya Akili Unde katika sekta za kimkakati kama elimu na afya.
Waziri Kairuki alieleza kwa kina kuhusu uwekezaji unaoendelea wa Serikali katika miundombinu ya kidijitali, akitaja upanuzi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano (NICTBB) pamoja na maendeleo ya Miundombinu ya Umma ya Kidijitali (Digital Public Infrastructure – DPI) kama msingi muhimu wa kupanua mawasiliano ya kidijitali na kuwezesha wananchi wengi zaidi kupata huduma zinazotumia Akili Unde nchini kote.
Akihitimisha hotuba yake, Waziri Kairuki alitoa wito wa kuimarishwa kwa ushirikiano wa kimataifa katika uhamishaji wa teknolojia, maendeleo ya ujuzi, ushirikiano wa tafiti, ubunifu na uwekezaji katika miundombinu ya kidijitali.
Mdahalo wa Kimataifa kuhusu Utawala wa Akili Unde unawakutanisha watunga sera, viongozi wa serikali, wataalamu wa teknolojia na wadau wa sekta binafsi kutoka duniani kote kwa lengo la kujenga mifumo ya kimataifa ya utawala wa Akili Unde na kujadili namna teknolojia hiyo inavyoweza kuchangia maendeleo jumuishi na endelevu.
