Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

“TUFANYE MAZOEZI KUEPUKA MAGONJWA YASIYOAMBUKIZA” – NAIBU KATIBU MKUU ABDULLA


Na Mwandishi Wetu, WHMTH, Dodoma

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Bw. Mohammed Khamis Abdulla leo Januari 28, 2023 ameshiriki mazoezi na watumishi wa Wizara hiyo yaliyofanyika katika viwanja vya Magereza jijini Dodoma na kuwashauri watumishi kuwa na utamaduni wa kufanya mazoezi ili kujiepusha na magonjwa yasiyoambukiza.

“Tukifanya mazoezi hata maradhi yanayotokana na uchovu au msongo wa mawazo yatapungua”, amesisitiza Bw. Abdulla

Aidha amewashauri watumishi wa Wizara hiyo kujenga timu imara ya mazoezi na ikiwezekana kila jumamosi asubuhi watumishi wawe na muda mchache wa kufanya mazoezi.

“Tujenge timu imara ya michezo ili kuchangamsha mwili na akili baada ya kazi, binafsi nitakuwa mshiriki kwa kuwa napenda mazoezi”, alisisitiza Bw. Abdulla.

Naye Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa Wizara hiyo, Bi Teddy Njau amesema kuwa mazoezi yaliyofanyika leo ni mwanzo wa mpango wa Wizara hiyo kufanya mazoezi kila jumamosi ya mwisho wa mwezi ili kuimarisha afya ya mwili.

“Taasisi yeyote ili itekeleze majukumu yake vizuri lazima watumishi wawe na afya bora ambayo haipatikani kupitia lishe pekee bali na kuhakikisha pamoja na utekelezaji wa majukumu wanapata muda wa kufanya mazoezi  ambayo pamoja na kuimarisha afya ya mwili pia yatazidi kutuweka pamoja “, amezungumza Bi. Njau