Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

TTCL NA HUAWEI ZASAINI MKATABA WA BILIONI 37.4 WA UPANUZI WA MKONGO WA TAIFA WA MAWASILIANO WASAINIWA


Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Nape Moses Nnauye (Mb) akizungumza akiwa Mgeni rasmi katika hafla ya utiaji saini mkataba wa upanuzi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano katika wilaya 23 nchini baina ya Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) na HUAWEI Tanzania leo Aprili 17, 2023 jijini Dodoma

 

Na Mwandishi Wetu, WHMTH, DODOMA

Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) na Kampuni ya HUAWEI International imesaini mkataba wa shilingi bilioni 37.4 wa upanuzi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano katika wilaya 23 nchini kwa lengo la kuunganisha Makao makuu ya mikoa na wilaya.

 

Utiaji saini huu umefanyika leo Machi 17, 2023 jijini Dodoma baada ya Serikali kuhamishia shughuli zote za muundombinu wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano kuhamishiwa katika Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) ikiwepo ujenzi, uendeshaji na usimamizi wa muundombinu huo.


Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye (Mb) ameshuhudia tukio hilo na kuwataka Shirika la TTCL kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa mujibu wa mkataba kwa kuzingatia ubora na muda wa kukamilika kwa mradi.

 

Amesema kuwa wilaya 23 zinazoenda kuunganishwa kwenye Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano zinaenda kuwa na mawasiliano bora na yenye uhakika ambayo yatasaidia katika shughuli za maendeleo na ujenzi wa Taifa letu, kukuza matumizi ya TEHAMA na kuongeza kasi upatikanaji wa Intaneti yenye kasi.


“Kwenye uchumi kila ongezeko la watumiaji wa mtandao wenye kasi (broadband) kwa asilimia 10 inasababisha ongezeko la pato la taifa kwa asilimia 2.5. Uwekezaji huu ni faida kubwa kwa ukuaji uchumi wa nchi yetu.

 

Waziri Nnauye amesema kuwa malengo ya Wizara ni kuhakikisha Makao Makuu ya Mkoa na Wilaya yameunganishwa na Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano ili kuimarisha mawasiliano ya ndani na kutoa fursa kwa Sekta ya Umma na Binafsi kufikisha huduma zao kwa wananchi kwa haraka na ubora unaohitajika.

 

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya TTCL, Bi. Zuhura Muro amesema kuwa Shirika hilo lina uwezo na limejipanga kukamilisha miradi kwa wakati na ubora mkubwa kwa maslahi ya Taifa na kutimiza lengo la Serikali la kuelekea katika uchumi wa kidijiti.

 

Kwa upande wa Kaimu Katibu Mkuu na Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa Wizara hiyo, Bi. Salome Kessy amelipongeza Shirika hilo kwa kazi nzuri inayoifanya ya utekelezaji wa mkakati wa upanuzi wa Mkongo wa Taifa mpaka ngazi ya wilaya ambapo kilomita 1,520 za Mkongo zinaenda kujengwa na kuunganisha wilaya 23.

Awali akizungumzia mkataba huo, Mkurugenzi Mkuu wa TTCL, Mhandisi Peter Ulanga amesema kuwa Wilaya hizo 23 ambazo zitakuwa katika mradi huu wa upanuzi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano ni pamoja na Msalala na  Mbogwe, Pangani ,Muheza, Kilindi, Mombo na  Lushoto, Ngara, Mwanga, Hai, Karatu, Longido, Mbulu,  Kibiti, Mtama, Ruangwa, Nachingwea, Newala, Mbinga, Ludewa, Viwawa na Ileje.

 

Ameongeza kuwa ujenzi huo kwa mujibu wa mkataba utatekelezwa katika kipindi cha miezi 6, ambapo Mkurugenzi Mtendaji wa HUAWEI Tanzania, Damon Zhang amethibitisha kuwa mradi huo utakamilika kwa wakati na watafanya kazi kwa kujitoa ili kuhakikisha Tanzania inakuwa kitovu cha mawasiliano katika ukanda wa Afrika Mashariki.