Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

Kamati ya Bunge Yakagua  Utekelezaji wa Mradi wa Minara 758 na Maabara ya Kisasa ya TCRA, Serikali Yasisitiza Mawasiliano Kufika Kila Kona ya Tanzania ifikapo 2030


Na Mwandishi wetu - WMTH Dar-es-salaam 

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Selemani Kakoso, leo Machi 18, 2026 ameiongoza Kamati ya Kudumu ya  Bunge ya Miundombinu katika ziara  ya ukaguzi wa utekelezaji wa miradi ya mawasiliano ikiwemo ujenzi wa minara 758 pamoja na maabara ya uidhinishaji wa vifaa vya kielektroniki ya TCRA, jijini Dar es Salaam. Ziara hiyo imelenga kujiridhisha na maendeleo ya miradi hiyo muhimu kwa sekta ya mawasiliano nchini.

Akizungumza katika ziara hiyo, Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Angellah Jasmine Kairuki, amesema kuwa serikali imefanikiwa kujenga minara sita katika Wilaya ya Kigamboni ikiwa ni sehemu ya mradi mkubwa wa minara 758 ulioanza Mei/13/2023. Ameeleza kuwa mradi huo umegharimu takribani shilingi bilioni 126 kwa kushirikiana na watoa huduma wa mitandao nchini.

Waziri Kairuki, Amefafanua kuwa katika Wilaya ya Kigamboni, minara hiyo imejengwa katika maeneo ya Kibada (Mtaa wa Kifurukwe), Kimbiji, Kisarawe II pamoja na Vijibweni, hatua ambayo imeongeza upatikanaji wa huduma za mawasiliano kwa wananchi wa maeneo hayo. Aidha, amesisitiza dhamira ya serikali kuhakikisha mawasiliano yanafika kila kona ya nchi ifikapo mwaka 2030.

Kwa upande mwingine, Waziri Kairuki ameongeza kuwa jumla ya minara 304 imeboreshwa kutoka teknolojia ya 2G hadi kufikia 4G na 5G, jambo linaloimarisha ubora wa huduma za mawasiliano na kuongeza kasi ya upatikanaji wa intaneti nchini. Hatua hii inaendana na juhudi za serikali za kukuza uchumi wa kidijitali.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mwenyekiti wa Kamati, Mhe. Kakoso, amesema lengo kuu la ukaguzi huo ni kujiridhisha na utekelezaji wa mradi wa minara 758 uliosainiwa Mei/13/2023. Ameipongeza serikali kwa juhudi zake za kupeleka huduma za mawasiliano katika maeneo ya vijijini ambayo hapo awali hayakuwa na mvuto kwa wawekezaji.

Ameongeza kuwa kamati inaomba miradi mingine ya mawasiliano inayoendelea itekelezwe kwa kasi zaidi ili wananchi wanufaike kwa wakati. Pia amewataka wananchi kuitunza miundombinu hiyo kwa kuwa walinzi wa kwanza, huku akiitaka wizara kuhakikisha ubora wa huduma na minara hiyo unazingatia viwango vinavyotakiwa.

Kwa upande wa utekelezaji wa miradi, Mkurugenzi Mkuu wa UCSAF, Eng. Peter Mwasalyanda, amesema kuwa ujenzi wa minara yote 758 umekamilika kwa asilimia 100, sambamba na uboreshaji wa minara 304 kutoka 2G hadi 4G na 5G. Ameeleza kuwa kwa sasa wanaendelea na ukaguzi wa kuhakikisha ubora na utendaji wa minara hiyo kote nchini, huku mnara wa Kigamboni ukitarajiwa kuhudumia wananchi zaidi ya 28,000.

Aidha, Mkurugenzi wa TCRA, Jabir Bakar, ameiongoza kamati hiyo kukagua maabara ya kisasa ya uidhinishaji wa vifaa vya kielektroniki iliyopo makao makuu ya mamlaka hiyo. Ameeleza kuwa maabara hiyo, ambayo imekuwa ikifanya kazi kwa zaidi ya miaka miwili, tayari imefikia viwango vya teknolojia ya 5G na ina uwezo wa kupima na kuthibitisha ubora wa vifaa mbalimbali vya mawasiliano kabla ya kuingia sokoni. Maabara hiyo inachangia kwa kiasi kikubwa kulinda ubora wa vifaa vinavyotumika nchini, kukuza ubunifu wa teknolojia na kuhakikisha Tanzania inaendana na kasi ya mapinduzi ya kidijitali duniani.