Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

Timu ya Wataalamu wa TEHAMA na Taasisi za Serikali Imefanya Ziara ya Mafunzo Nchini Thailand Kuhusu Uchumi wa Kidijitali


Timu ya wataalamu kutoka Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Wizara ya Fedha, Benki Kuu ya Tanzania (BOT), Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) pamoja na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) walifanya ziara ya mafunzo nchini Thailand, yenye lengo la kujifunza na kubadilishana uzoefu kuhusu uandaaji wa Akaunti ya Uchumi wa Kidijitali (DESA). Hatua hii ni muhimu katika kuimarisha ukusanyaji na uchambuzi wa takwimu za uchumi wa kidijitali nchini Tanzania.

 

Katika ziara hiyo, wataalamu waliongozwa na Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya TEHAMA, Dkt. Nkundwe Mwasaga, na walipata fursa ya kutembelea Taasisi ya Big Data (Big Data Institute – BDI), ambapo walijifunza mbinu za kisasa za ukusanyaji, uchambuzi, na matumizi ya big data katika shughuli za kiuchumi na kijamii.

 

Aidha, wataalamu walitembelea ofisi ya Kamati ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (Personal Data Protection Committee – PDPC) na kujifunza mifumo ya ulinzi, usimamizi na matumizi salama ya taarifa binafsi, uzoefu unaotarajiwa kusaidia Tanzania kuimarisha sera na mifumo ya usalama wa taarifa katika enzi ya uchumi wa kidijitali.