Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

TEKNOLOJIA KURAHISISHA UPATIKANAJI WA HUDUMA ZA POSTA NCHINI


Na Chedaiwe Msuya, WHMTH, Dar es Salaam.

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Moses Nnauye (Mb) amelipongeza Shirika la Posta nchini kwa ubunifu wake wa huduma ya Posta Kiganjani itakayorahisisha huduma za kijamii na kuisaidia Serikali kuongeza ukusanyaji wa mapato.

Waziri Nape amesema hayo wakati wa kilele cha Kongamano la Maadhimisho ya Siku ya Posta Duniani lenye kauli mbiu “Posta kwa Kila Mtu” lililofanyika jijini Dar es Salaam Oktoba 9, 2022.  

Muundombinu wa Posta Kiganjani utawezesha wananchi wengi kujihudumia wenyewe na kunufaika na huduma za posta mahali popote pale walipo. 

“Wakati nasikiliza maelezo ya posta kiganjani, nimegundua pia kuwa huduma hii imeingizwa kwenye mfumo wa malipo ya Serikali yaani GPeG, ambapo kimsingi kupitia huduma hii, Serikali itaongeza mapato moja kwa moja hivyo kuongeza pato la Taifa na kasi ya ukuaji wa uchumi,” amesema Waziri Nnauye.

Alieleza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi wa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan inahitaji ubunifu katika sekta mbalimbali nchini ili kuendana na kasi ya ukuaji wa teknolojia na kurahisisha huduma mbalimbali za kijamii.

Waziri Nape ametoa wito kwa Menejimenti ya Shirika la Posta nchini kuongeza nguvu kwenye vikundi vinavyoendana na mageuzi ya teknolojia ili kukidhi mahitaji mapya ya wateja yanayobadilika mara kwa mara, hususan biashara mtandao na kuwataka Watanzania kutumia huduma za Shirika hilo.  

Kwa upande wake, Postamasta Mkuu wa Shirika la Posta nchini Bw. Macrice Mbodo amesema kuwa Posta Kiganjani imegusa maeneo mengi ya kijamii na kiuchumi ikiwa ni pamoja na sekta ya elimu, afya, uchumi na biashara, huduma za Kiserikali na usafirishaji na kusaidia Jeshi la Polisi nchini kudhibiti usafirishwaji wa vifaa vya kivita na madawa ya kulevya nchini.

Amesema kuwa huduma za Posta Kiganjani pia zimezingatia matumizi rafiki ya TEHAMA ili kurahisishia wateja upatikanaji wa huduma wanazohitaji popote walipo.

Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Posta Duniani kilihudhuriwa na watu zaidi ya 300, akiwemo Balozi wa Posta nchini mwanamuziki na msanii Mrisho Mpoto.