Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

TEHAMA KUIBUA FURSA ZA AJIRA NA KULETA MAENDELEO YA KIUCHUMI KWENYE JAMII


Na Chedaiwe Msuya, Dar es Salaam

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye (Mb) amewataka wadau wa TEHAMA kuwapa nafasi watu wa makundi maaluum katika maboresho ya teknolojia kwa kusikiliza maoni yao.

Hayo ameyasema leo octoba 18 jijini Dar es salaam wakati akifungua kongamano la 7 la TEHAMA linalofanyika kwa siku 5 katika ukumbi wa kimataifa wa mikutano wa Julius Nyerere JNICC.

Amesema kongamano hilo limezingatia ushiriki wa makundi yote ikiwemo vijana na wanawake.

"Nimeona kwenye majadiliano mmeweka siku maalumu kwa ajili ya wanawake na vijana hii ni nzuri kwani ripoti ya Dunia inaonyesha ushiriki wa wanawake kwenye TEHAMA ni mdogo basi kongamano lijalo muangalie namna ya kuwahusisha watu wenye makundi maalum wakiwemo walemavu"amesema.

Amesema serikali imeingia makubaliano na serikali ya India katika kuboresha TEHAMA hivyo wanapaswa kutumia fursa ya makubaliano hayo katika kujijengea uwezo na kupata uzoefu ili kuifanya nchi kuwa kitovu cha teknolojia bunifu.

Amesema mafanikio hayo yanalenga kufikia maono yalionyeshwa kwenye mkakati wa uchumi wa kidigitali ambao umeandaliwa na Wizara kwa kushirikiana na ofisi za umma na binafsi ambapo mkakati huo upo kwenye hatua za mwisho kupelekwa kwenye maamuzi.

Aidha Mhe. Nape ameongeza kuwa kufanya ushirikiano na nchi zilizopiga hatua kutasaidia kuiwezesha nchi kusonga mbele kwenye matumizi ya teknolojia.

"Tunayo kila sababu ya kufanikiwa kwenye TEHAMA kwani mazingira tuliyonayo,miundombinu,utashi wa kisiasa uliopo,uwekezaji uliowekwa kwenye miundombinu hatuna sababu ya kubaki nyuma"amesema Mhe. Nape.

Amesema matumizi ya teknolojia inayoibukia inawezeshwa pamoja na miundombinu rafiki ambapo serikali inatambua juhudi zinazofanywa na sekta binafsi katika ujenzi wa miundombinu hiyo ya mawasiliano.

"Hivi karibuni tumesaini leseni nne za data centers hii inaonyesha ni kwa jinsi gani wawekezaji wanalizika na mazingira yaliyowekwa nchini katika kuhakikisha sekta ya Tehama inakua na ongezeko lake linaenda kugusa maisha ya watu"ameongeza.

Mhe. Nape pia amesema juhudi za makusudi zinapaswa kuchukuliwa ili kuhakikisha hakuna anaeachwa na teknolojia hiyo ili kuleta uchumi jumuishi wa kidigital.

Amesema takwimu za watumiaji wa internet zimeongezeka kutoka milioni 29.9 mwezi Aprili 2022 hadi milioni 34.04 mwezi juni 2023 ambapo ni Sawa la ongezeko la asilimia 13.8.

"Mafanikio haya yanaenda sambamba na uhitaji wa wananchi kuelimishwa kuhusu usalama wa mitandao na namna gani wanaweza kujilinda kutumia mitandao hii kwa manufaa yao wenyewe"amesema.

"Matumizi ya Teknolojia zinazoibukia yanaenda sambamba na uhatarishi wa taarifa zetu binafsi hivyo jambo la msingi watumiaji wa huduma kufuata maelekezo ya wataalam"ameongeza.

Kwa upande Mbunge wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu Mhe. Livingstone Lusinde amesema Bunge litaendelea kuunga mkono juhudi zinazofanywa kwa kuchambua miswada mbalimbali ya kisheria itakayopelekwa bungeni lakini pia kupitisha ongezeko la bajeti kwa wizara hiyo.

Naye, Naibu Waziri  wa Wizara ya Habari Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Eng. Andrew Kundo amemshukuru Rais Dk.Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuweka mazingira rafiki katika ukuaji wa Sekta ya TEHEMA ndani ya nchi lakini pia kuvutia uwekezaji katika sekta hiyo.

Kongamano la 7 la TEHAMA ambalo litafanyika kwa muda siku tano linatumika kama jukwaa muhimu kwa wadau wote wa TEHAMA kubadilishana mawazo uzoefu na kuibua fursa zilizopo hivyo linatarajiwa kutoka maazimio ambayo yataishauri serikali namna bora ya kuwezesha sekta hiyo katika ukuaji wa uchumi wa kidigitali ambapo kauli mbiu ya mwaka huu inasema "kutumia teknolojia ibukizi katika mapinduzi ya kidigitali ili kuzalisha ajira na kuleta maendeleo ya kiuchumi na kijamii"