Habari
TEHAMA CHACHU YA BIASHARA NA UWEKEZAJI
Na Mwandishi Wetu, WHMTH, Dar es Salaam
Uwekezaji wenye tija katika TEHAMA imekuwa ni chachu ya kuongeza uzalishaji, ufanisi na kuchochea suluhisho bunifu katika sekta zote nchini na kuifanya Tanzania kuwa sehemu bora kwa biashara na uwekezaji wa ndani na wa kimataifa.
Hayo yamesemwa na Bw. Mulembwa Munaku, Mkurugenzi wa Idara ya Huduma za Mawasiliano wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari wakati wa Kongamano la Uhusiano na Biashara kati ya Tanzania na Malaysia lililofanyika tarehe 21 hadi 22 Novemba, 2024 katika Hoteli ya Serena, jijini Dar es Salaam.
Bw. Munaku ameuzungumzia Mkakati wa Taifa wa Uchumi wa Kidijitali wa mwaka 2024–2034 kuwa una nguzo sita zinazotoa dira ya ukuaji jumuishi wa uchumi wa kidijitali ambazo ni miundombinu ya kidijitali; ujuzi na maarifa ya kidijitali; Bunifu na biashara za kidijitali; huduma za umma kidijitali; huduma za fedha kidijitali na Ujumuishaji wa maunganisho ya kidijitali.
Ameongeza kuwa, nchi ya Tanzania imepiga hatua katika kukuza matumizi ya TEHAMA lakini bado ni muhimu kuwa na ushirikiano wa kibiashara na ubia na sekta binafsi wenye nguvu ya kutoa suluhisho kupitia TEHAMA katika utoaji wa huduma za sekta zote za uchumi.
“Malaysia inajulikana kwa utaalam wake katika TEHAMA, hivyo kuna haja kubwa ya kuwekeza au kushirikiana kibiashara baina ya makampuni ya Tanzania na Malaysia katika maeneo sita ikiwemo kupanua wigo wa mtandao wa mawasiliano katika maeneo yaliyosahaulika na kuboresha uzalishaji wa maudhui ya kidijitali”, amesema Bw. Munaku.
Maeneo mengine aliyoyazungumzia ni kuboresha bunifu za TEHAMA zitakazoleta ushindani katika huduma za usafirishaji na posta; kuingia ubia wa kukuza uchumi wa kidijitali Tanzania kupitia biashara mtandao na suluhisho za kifedha za kidijitali, kuharakisha maendeleo ya suluhisho bunifu za TEHAMA na wataalamu kubadilishana uzoefu sambamba na mabadiliko ya kiteknolojia.
Kongamano hilo limezikutanisha Kampuni za Watanzania zinazojishughulisha na masuala ya TEHAMA na kampuni kutoka Malaysia kupitia Shirika la Uchumi wa Kidijitali la Malaysia (MDEC) ambapo walipata nafasi ya kubadilishana uzoefu na ujuzi na kujadili njia bora za ushirikiano katika TEHAMA.