Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

TANZANIA YAVUTIA WAWEKEZAJI WA KIJAPANI KWENYE SEKTA YA TEHAMA


Mkurugenzi wa Mawasiliano kutoka Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Bw. Mulembwa Munaku (mwenye suti ya kijivu aliyeketi) akiwa katika picha ya pamoja na makundi mbalimbali ya washiriki wa Jukwaa la Biashara na Uwekezaji Kati ya Tanzania na Japani tarehe 09 Oktoba, 2025.

Na Mwandishi Wetu, WMTH, Tokyo

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imesisitiza dhamira yake ya kuendeleza ushirikiano na Japani katika kukuza sekta ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ili kuimarisha uchumi wa kidijitali na kuvutia wawekezaji wapya kupitia ubunifu na teknolojia za kisasa.

Kupitia Jukwaa la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Japani lililofanyika Oktoba 9, 2025 jijini Tokyo, Tanzania imekaribisha wawekezaji wa Kijapani kushirikiana katika kuendeleza miundombinu ya TEHAMA, ubunifu wa kidijitali, na uwekezaji unaolenga kuchochea ukuaji endelevu wa sekta ya teknolojia nchini.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa jukwaa hilo, Mkurugenzi wa Huduma za Mawasiliano kutoka Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Bw. Mulembwa Munaku amesema Tanzania ipo katika safari ya mageuzi ya kidijitali kupitia Mkakati wa Taifa wa Uchumi wa Kidijitali wa Miaka 10, unaolenga kutumia TEHAMA kama injini ya ukuaji wa uchumi na ubunifu.

Bw. Munaku ameeleza kuwa juhudi hizo zinaendana na Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 na Ajenda ya Umoja wa Mataifa ya SDGs, zikilenga kujenga uchumi jumuishi unaotumia teknolojia kuboresha huduma kwa wananchi.

Matumizi ya simu za mkononi yamefikia zaidi ya asilimia 90 na huduma za kifedha za kidijitali zimebadilisha maisha ya Watanzania, huku Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano ukiifanya Tanzania kuwa kitovu muhimu cha kidijitali katika Afrika Mashariki na Kati, alielezea Bw. Munaku.

Amesema kuwa, ukuaji wa kampuni changa za teknolojia umefikia asilimia 24 mwaka 2024 na kuonesha mwamko mkubwa wa ubunifu unaoongozwa na vijana, ambapo zaidi ya asilimia 60 ya Watanzania wako chini ya umri wa miaka 25 na wana ari ya kutumia teknolojia kuleta mabadiliko chanya.

Aidha, Bw. Munaku imeainisha maeneo ya ushirikiano yanayotarajiwa kati ya Tanzania na Japani kama miradi ya miji janja, miundombinu ya 5G, fintech, biashara mtandaoni, usalama wa mtandao, na teknolojia za satelaiti na anga, akisisitiza kuwa uchumi wa kidijitali unahusu zaidi ya teknolojia pekee bali ni chachu ya maendeleo jumuishi na ustawi wa pamoja.