Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

TANZANIA YASHIRIKI UFUNGUZI WA MKUTANO WA 44 WA BARAZA LA UTAWALA LA UMOJA WA POSTA AFRIKA (PAPU)


Na Mwandishi wetu -WMTH
Kampala, Uganda.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Bw. Nicholas Merinyo Mkapa, ameongoza Timu ya Wataalam kutoka Tanzania katika Mkutano wa 44 wa Baraza la Utawala la Umoja wa Posta Afrika (PAPU), uliofanyika jijini Kampala, Uganda tarehe 23 Machi 2026. mkutano huo uliojumuisha Makatibu Wakuu kutoka katika Sekta ya Posta Barani Afrika. 

Ufunguzi wa mkutano huo ulifanywa na Dkt. Aminah Zawedde, Katibu Mkuu wa Wizara ya Teknolojia ya Habari na Mwongozo wa Kitaifa wa Uganda. Mkutano huu wa 44 wa Baraza la PAPU unafanyika kwa mujibu wa ratiba ya vikao vya Baraza vinavyokutana kabla ya Mkutano Mkuu wa Mawaziri wenye dhamana ya Sekta ya Posta Barani Afrika ambao ni Mkutano wa 11, unaotarajiwa kufanyika kuanzia tarehe 25 hadi 27 Machi 2026.

Mkutano wa 44 wa Baraza la PAPU umejumuisha viongozi na wataalam mbalimbali wa Sekta ya posta, wakiwemo Makatibu Wakuu, Wakurugenzi wa mamlaka za udhibiti, wakuu wa taasisi za posta pamoja na wataalam wa Sekta hiyo kutoka nchi mbalimbali za Afrika.

Kwa upande wa Tanzania, ujumbe umejumuisha wawakilishi kutoka Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Wizara ya Mawasiliano, Teknolojia ya Habari na Ubinifu ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) pamoja na Shirika la Posta Tanzania. (TPC)