Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

TANZANIA YASHINDA NAFASI MUHIMU KATIKA UMOJA WA POSTA DUNIANI (UPU)


Tanzania imepata ushindi mkubwa katika uchaguzi wa kupata nafasi za ujumbe kwenye mabaraza mawili muhimu ya Umoja wa Posta Duniani (UPU), hatua inayoonesha mchango na umahiri wake katika sekta ya mawasiliano ya posta duniani.

Uchaguzi huo ulifanyika Septemba 18, wakati wa Mkutano Mkuu wa 28 wa UPU unaoendelea mjini Dubai, Falme za Kiarabu. Katika uchaguzi huo, Tanzania ilifanikiwa kushinda nafasi ya tano ya ujumbe kwenye Baraza la Uendeshaji wa Posta baada ya kupata kura 123. Kati ya nafasi 11 zilizokuwa zinashindaniwa, nchi zilizopata kura nyingi zaidi ya Tanzania ni Misri (135), Algeria na Morocco (129 kila moja), pamoja na Kenya (127).

Aidha, Tanzania pia imeibuka mshindi wa nafasi kwenye Baraza la Utawala, ambapo kati ya nchi 11 zilizochaguliwa, Tanzania ilipata kura 132 na kushika nafasi ya pili, nyuma ya Misri iliyopata kura 133.
Ushindi huu katika  Baraza la Utawala unaipa Tanzania nafasi ya kushiriki moja kwa moja katika kufanya maamuzi ya kimataifa kuhusu mwelekeo na sera za sekta ya posta.

Kupitia ushindi huu, Tanzania imetambuliwa rasmi kwa mchango wake katika kuendeleza huduma za posta barani Afrika na duniani na pia ni  fursa kwa nchi kushiriki kikamilifu katika majadiliano ya kimkakati kuhusu mageuzi ya huduma za posta katika zama za kidijitali.