Habari
TANZANIA YASAINI MKATABA WA UMOJA WA MATAIFA DHIDI YA UHALIFU WA MTANDAONI
Na Mwandishi Wetu, WMTH, Hanoi, Vietnam
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeungana na mataifa mengine duniani kusaini Mkataba wa Umoja wa Mataifa Dhidi ya Uhalifu wa Mtandaoni, ikionesha dhamira thabiti ya kuimarisha usalama wa kidijiti na kupambana na vitendo vya kihalifu vinavyofanywa kupitia mtandao.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Bw. Mohammed Khamis Abdulla, alimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika hafla ya utiaji saini iliyofanyika tarehe 25 Oktoba 2025 jijini Hanoi, Vietnam, akiambatana na Balozi wa Tanzania nchini China Mhe. Khamis Mussa Omar pamoja na maafisa waandamizi kutoka Wizara na taasisi mbalimbali za Serikali.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Rais wa nchi mwenyeji ya Vietnam, Mhe Luong Cuong, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres na wawakilishi kutoka zaidi ya mataifa 100 duniani, yaliyoweka saini zao kuunga mkono mapambano dhidi ya uhalifu wa mtandaoni.
Akizungumza baada ya hafla hiyo, Bw. Abdulla aliipongeza Kamati Maalumu ya Umoja wa Mataifa kwa kufanikisha maandalizi ya Mkataba huo kupitia majadiliano yaliyochukua zaidi ya miaka mitano, akiyataja kuwa ushindi wa kidiplomasia na ushahidi wa mshikamano wa kimataifa katika kulinda usalama wa mtandao.
Amesema mchakato wa kufikia makubaliano hayo ulikuwa mgumu lakini wenye mafanikio, kutokana na ukomavu wa nchi wanachama wa umoja huo katika kufanya maridhiano na kuweka mbele maslahi ya dunia nzima.
Bw. Abdulla amepongeza pia uwepo wa masharti ya kujengewa uwezo na kusaidiwa kiteknolojia kwa nchi zinazoendelea ili ziweze kukabiliana ipasavyo na wimbi linaloongezeka la uhalifu wa kimtandao.
Aidha, Bw. Abdulla amepongeza vipengele vya mkataba huo vinavyohusu ushirikiano wa kimataifa katika ukusanyaji, uhifadhi na ubadilishanaji wa ushahidi wa kielektroniki, akisema utarahisisha uchunguzi wa makosa ya kimtandao kwa ufanisi.
Amebainisha kuwa Tanzania itatoa tamko maalum wakati wa kuridhia mkataba huo ili kuhakikisha utekelezaji wake unazingatia misingi ya kisheria na maadili ya Tanzania.
Akihitimisha, Bw. Abdulla amesisitiza dhamira ya Tanzania kushirikiana na jumuiya ya kimataifa katika vita dhidi ya uhalifu wa mtandao, akisema ni jukumu la pamoja linalohitaji mshikamano wa mataifa yote kwa usalama wa kidijiti duniani.
