Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

TANZANIA YAPOKEA TUZO YA MFUKO WA UBORA WA HUDUMA KUTOKA UMOJA WA POSTA DUNIANI (UPU)


Umoja wa Posta Duniani (UPU) kupitia Mfuko wa Ubora wa Huduma (Quality of Service Fund-QSF) Umetoa Tuzo ya Ubora kwa Shirika la Posta Tanzania kutokana na kuandaa, kusimamia na kutekeleza kikamilifu Mradi namba QSFTZA1509 wenye thamani ya dola za Marekani ($328,000) sawa na fedha za kitanzania milioni 849,520,000 kwa ajili ya ununuzi wa magari 6 (3.5 Ton trucks) ili kuwezesha Usafirishaji wa barua, vifurushi na vipeto katika njia ya Dar-Singida na Singida-Mwanza na Kigoma.
 
Tuzo hiyo imetolewa leo tarehe 26 Aprili, 2024 jijini Berne, Uswisi Makao Makuu ya Umoja wa Posta Duniani na kupokelewa na Bwana Mulembwa Munaku, Mkurugenzi wa Mawasiliano, Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari pamoja na Bwana Constantine Kasese, Mkurugenzi wa Biashara Mtandao na Huduma za Fedha na Uwakala aliyemuwakilisha Postamasta Mkuu Bwana Maharage Chande.
 
Tuzo hizo zimetolewa na Mkurugenzi Mkuu wa UPU, Bwana Masahiko Metoki, Mwenyekiti wa Bodi ya Mfuko huo Bwana Aime Thaubet wa Uswisi pamoja na Mwenyekiti wa Baraza la Uendeshaji la UPU Bwana Jean Paul Forceville wa Ufaransa.
 
Nchi nyingine zilizopokea tuzo hizo ni pamoja na Malaysia, Argentina, El Salvado, Panama, Kazakhstan, Ukraine, Vietnam, Colombia, Bulgaria, Guyana, Niger na Cape Verde.
 
Kwa pamoja nchi hizo zimepongezwa kwa kuwa mfano wa utekelezaji wa miradi hiyo kwa ubora wa hali ya juu.

 
Imetolewa na;
Kurugenzi ya Masoko na Uhusiano,
Shirika la Posta Tanzania.