Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

TANZANIA YAPENDEKEZA KUANZISHWA KWA MFUMO WA UFUATILIAJI NA TATHMINI WA ATHARI ZA TEHAMA


Na Mwandishi Wetu, WMTH Geneva Uswisi

Tanzania inashiriki Mkutano wa 28 wa Kamisheni ya Sayansi na Teknolojia kwa Maendeleo ulioanza tarehe 7 Aprili 2025 na unatarajia kuhitimishwa tarehe 11 Aprili, 2025 katika jiji la Geneva, Uswisi. Mkutano huu umezikutanisha nchi wanachama kwa lengo la kuwasilisha taarifa za utekelezaji wa masuala ya sayansi, teknolojia na ubunifu katika kuleta maendeleo.

Ujumbe wa Tanzania umeongozwa na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Omary Juma Kipanga (Mb). ambaye ameambatana na Bw. Mohammed Khamis Abdulla, Katibu Mkuu Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, na Bi. Hawwah Ibrahim Mbaye, Naibu Katibu Mkuu wa Mawasiliano kutoka Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi kutoka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar pamoja na wataalamu mbalimbali.  

Katika mkutano huo Serikali ya Tanzania imependekeza kuanzishwa kwa mfumo wa kimataifa wa ufuatiliaji na tathmini wa athari za Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika maendeleo endelevu na haki za binadamu, pamoja namna ya kukabiliana na mabadiliko ya mazingira ya kidijitali na athari zake kimataifa.

Mapendekezo hayo yamewasilishwa na Naibu Katibu Mkuu wa Mawasiliano kutoka Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Zanzibar, Bi. Hawwah Mbaye wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa nchi wa malengo ya jamii habari (WSIS Action Lines) wakati wa Mkutano wa 28 wa Kamisheni ya Sayansi na Teknolojia kwa Maendeleo (Commission of Science, Technology for Development – CSTD).

Aidha, katika taarifa hiyo Serikali ya Tanzania imesema kuwa itaendelea kujenga Taifa la kidijitali kupitia utekelezaji wa Mkakati wa Uchumi wa Kidijitali (2024–2034) unaolenga kuharakisha matumizi ya Teknolojia ya TEHAMA katika sekta zote za uchumi ili kuleta mabadiliko chanya katika utoaji wa huduma za umma, kuimarisha ubunifu, na kupunguza pengo la kijamii kati ya maeneo ya mijini na vijijini.

Bi. Mbaye ametaja moja ya mafanikio makubwa ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni uanzishaji wa jukwaa la Kitaifa la Jamii X-Change, linalowezesha mifumo ya TEHAMA ya kisekta mbalimbali kuweza kusomana na kubadilishana taarifa hivyo kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi. 

Kwa upande wa miundombinu ya TEHAMA, Tanzania imepiga hatua kubwa kwa kuunganisha wilaya 109 kati ya 139 na Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano huku matarajio ni kufikia asilimia 100 ya uunganishaji ifikapo mwisho wa mwaka 2025. 

Kwa upande wa huduma ya mawasiliano ya simu na Intaneti asilimia 88 ya wananchi wanapata huduma ambapo Serikali imechangia ujenzi minara ya mawasiliano 2,158 katika kata 1,974, na kufikisha huduma za kidijitali katika vijiji 5,111 vyenye jumla ya wakazi 23,799,848 wengi wao wakiwa katika maeneo ya vijijini na pembezoni mwa nchi.

Aidha katika kulinda usalama wa taarifa binafsi, Tanzania imetunga Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC) na kuanzisha Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC) ambayo inahusika katika kulinda faragha na usalama wa taarifa binafsi.

Serikali ya Tanzania imeeleza dhamira ya dhati ya kutekeleza makubaliano ya WSIS na makubaliano mengine ya kimataifa yanayosaidia kutoa suluhisho la changamoto za kidijitali kwa lengo la kufikia maendeleo endelevu ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano.