Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

Tanzania Yapanua Ushirikiano wa TEHAMA na Korea Kusini, Kuanzisha Chuo Mahiri cha TEHAMA Jijini Dodoma


Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Dkt. Switbert Zacharia Mkama (Mb), ameongoza ujumbe wa Tanzania katika ziara ya kikazi nchini Korea Kusini yenye lengo la kuimarisha na kudumisha ushirikiano wa kimkakati katika uanzishwaji wa Chuo Mahiri cha TEHAMA (National Digital Technology Institute – DTI), kinachotarajiwa kujengwa katika eneo la Nala, jijini Dodoma.

 

Katika ziara hiyo, Mhe. Dkt. Mkama na ujumbe wake walikutana na wadau muhimu wa utekelezaji wa mradi huo, wakiwemo viongozi wa Chuo Kikuu cha Hanyang, ambako walipata fursa ya kutembelea maabara za kisasa za Robotics na ubunifu wa kiteknolojia. Aidha, walifanya mazungumzo na Benki ya Korea kuhusu uwezeshaji wa kifedha kwa ajili ya ujenzi wa chuo hicho.

 

Kupitia ushirikiano huu, Tanzania na Korea Kusini zimekubaliana kushirikiana katika kujenga uwezo wa maandalizi ya wataalamu watakaohusika katika uendeshaji na ufundishaji ndani ya DTI, hatua inayolenga kuhakikisha chuo hicho kinakuwa kituo cha ubora katika TEHAMA na teknolojia za kidijitali.