Habari
TANZANIA YAONGOZA MAGEUZI YA MAWASILIANO YA ANGA KUPITIA JUKWAA LA PAMOJA LA SATELAITI YA SADC
Na Mwandishi Wetu, WMTH – Dar es Salaam
Tanzania inatambua kuwa anga na matumizi ya Teknolojia ya Satelaiti ni msingi muhimu katika miundombinu ya mawasiliano unaolenga kuboresha maendeleo ya kidijitali, ujumuishaji wa kikanda na uimarishaji wa usalama wa mawasiliano.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki (Mb), wakati wa hafla ya ufunguzi wa Mkutano wa Jukwaa la Pamoja la Satelaiti la Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) iliyofanyika tarehe 16 Februari, 2026 jijini Dar es Salaam.
Waziri Kairuki alibainisha kuwa Tanzania imenufaika kwa kiasi kikubwa kutokana na uwekezaji katika Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano (NICTBB) ambao umewezesha kuunganisha nchi jirani za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Malawi, Msumbiji na Zambia pamoja na ujenzi wa zaidi ya minara 2,151 ya mawasiliano kote chini ya Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF).
Aliongeza kuwa, hatua hizo zimeongeza upatikanaji wa huduma za mawasiliano nchini hadi kufikia asilimia 98.6 kwa 2G, 93.4 kwa 3G, 94.2 kwa 4G na 30.1 kwa 5G kufikia Desemba 2025.
Waziri Kairuki alieleza kuwa Tanzania inatekeleza Programu ya Taifa ya Anga (National Space Programme) ikiwemo Mradi wa KiboCube unaotekelezwa kwa ushirikiano na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Masuala ya Anga ya Nje ya Dunia (UNOOSA) na Wakala wa Utafiti wa Anga wa Japan (JAXA). Mradi huo unalenga kujenga uwezo wa kitaalam wa wazawa na kuhakikisha Tanzania inakuwa miongoni mwa nchi zinazoongoza katika teknolojia za satelaiti barani Afrika.
Mhe. Kairuki alisema kuwa Tanzania inajivunia kuwa mwenyeji wa majadiliano hayo muhimu yanayolenga kuboresha matumizi ya teknolojia ya satelaiti yatakayosaidia sekta nyingine kama kilimo, madini, mazingira, usalama na udhibiti wa majanga hivyo kuongeza tija katika uchumi wa Taifa na ustawi wa wananchi.
“Ni lazima tuhakikishe kwamba huduma za pamoja za satelaiti si tu zinakuwa imara kiteknolojia, bali pia zinakuwa endelevu kifedha, jumuishi, na salama. Tunapaswa kusonga mbele zaidi ya sera na kukamilisha mipango ya taasisi na mifumo ya utawala kwa ajili ya Mtandao wa Pamoja wa Satelaiti wa SADC,” alisema Waziri Kairuki.
Aidha, alisisitiza kuwa kupitia dira ya pamoja chini ya SADC Vision 2050 na Agenda 2063, nchi za Afrika zinaweza kuhakikisha hakuna mwananchi anayeachwa nyuma katika safari ya kidijitali.
Waziri Kairuki alitoa wito kwa nchi wanachama wa SADC kuendelea kushirikiana ili kuhakikisha teknolojia hizo zinakuwa endelevu, shirikishi na salama na kuongeza kuwa Jukwaa la Pamoja Satelaiti la SADC litajadili nafasi ya nchi hizo pamoja na uratibu wa huduma za satelaiti na maandalizi ya Mkutano wa Dunia wa Mawasiliano ya Redio utakaofanyika 2027 (WRC-2027).
