Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

TANZANIA YANADI MAFANIKIO YA MATUMIZI YA AKILI UNDE KATIKA MAGEUZI YA KIDIJITALI


Na Mwandishi wetu

Geneva, Uswisi.

 

Tanzania imewasilisha mafanikio yake katika matumizi ya Akili Unde (AI) na mageuzi ya kidijitali katika utoaji wa huduma za umma wakati wa Kongamano la Kimataifa kuhusu Jamii ya Habari (World Summit on the Information Society - WSIS Forum 2026) unaoendelea Geneva, Uswisi.

 

Akiwasilisha mada hiyo, Mkurugenzi wa Miundombinu na Uendeshaji wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA), Bw. Benjamin Dotto, alisema Tanzania imejenga msingi imara wa matumizi salama ya AI kupitia Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi ya mwaka 2022, Alieleza kuwa nchi imeunganishwa kwa zaidi ya kilometa 15,000 za Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano, huku akiongeza kuwa, nchi imefikia asilimia 95 ya huduma za mawasiliano ya simu na asilimia 82.6 ya matumizi ya intaneti, huku ikiwa imeendeleza mifumo 14 ya AI inayotumika na ambayo ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji.

 

Aidha, Serikali imewajengea uwezo wataalamu zaidi ya 500 wa TEHAMA, inaendelea kuendeleza matumizi ya Kiswahili katika AI kupitia hifadhidata yenye zaidi ya maneno milioni 61 na inashughulikia changamoto za upungufu wa wataalamu, gharama za teknolojia na miundombinu ya AI.

 

Naye Mkurugenzi Msaidizi wa Mifumo, Huduma za TEHAMA na Uzingatiaji kutoka Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Angelina Misso, alisema utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Uchumi wa Kidijitali wa miaka 10 umeimarisha ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi katika ujenzi wa miundombinu ya TEHAMA, maendeleo ya Akili Unde (AI), vituo vya kuhifadhi taarifa na ujenzi wa uwezo wa wataalamu, hatua ambazo zinaendelea kuiwezesha Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zinazoongoza mageuzi ya kidijitali barani Afrika.

 

Katika mjadala, Meneja wa Utafiti, Ubunifu na Mafunzo wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA), Dkt. Jaha Mvulla, alisema vijana ndio nguvu kubwa ya ubunifu wa kidijitali nchini, na Serikali inatoa kipaumbele kuhakikisha vijana wabunifu kwenye eneo la kidijitaliwanapata mazingira mazuri ya kuendelea bunifu zao na kuwa sehemu kukuza uchumi wa kidigiti.

 

Kupitia kituo cha Utafiti na Ubunifu cha Mamlaka ya Serikali Mtandao zaidi ya vijana 1,000 wamehusishwa kupitia mafunzo, programu za mafunzo kwa vitendo, na ushirikiano na vyuo vikuu ili kuendeleza suluhisho za kidijitali. Serikali Kupitia Mradi wa Tanzania ya Kidijitali inaendelea kujenga vituo zaidi vya Ubunifu ili kutoa fursa zaidi kwa vijana wabunifu wa kitanzania.