Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

TANZANIA YAJIPANGA KUPELEKA MIUNDOMBINU YA MAWASILIANO DRC


Na Innocent Mungy, Lubumbashi

Serikali ya Tanzania iko tayari kupeleka Miundombinu ya Mawasiliano katika nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kupitia Ziwa Tanganyika.

Hayo yamesemwa na Mhe. Nape Nnauye, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari akizungumza wakati wa ufunguzi wa Kongamano la Fursa za Kibiashara na Uwekezaji katika Sekta ya TEHAMA lililoanza leo jijini Lubumbashi.

Kongamano hili linafanyika miezi miwili tu tangu Viongozi wa nchi hizi mbili wakutane hapa DRC wakati wa ziara ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan.

“Serikali ya Tanzania iko tayari kuleta miundombinu ya mawasiliano ya Tanzania hususani Mkongo wa Taifa ili kuiunganisha DRC na nchi jirani. Tunaamini katika umoja na ushirikiano wa nchi zetu kushirikiana ili kufikia malengo ya kiuchumi ya nchi zetu na wananchi wetu kwa ujumla”, alisema Mheshimiwa Nape. 

Akizungumza katika Kongamano hilo, Balozi wa Tanzania nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Mhe. Balozi Said Mshana amewahakikishia wafanyabiashara na wawekezaji wa TEHAMA wa DRC kuwa Tanzania ni nchi iliyojipanga kufanya biashara na DRC.

“Tanzania na DRC ni soko la zaidi ya watu 160 na hivyo ushirikiano baini yetu ni muhimu, tukishirikiana pamoja tutakuwa na nafasi nzuri sana ya kuleta maendeleo kwa nchi zetu”, alisema Balozi Mshana.

Nae Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt. Jim Yonazi amewataka washiriki wa Kongamano hili kushiriki kwa ukamilifu kwenye majadiliano ili kuona fursa zilizopo baini ya Tanzania na DRC ili kubaini maeneo ya mashirikiano na kutumia fursa hizo.

Kongamano hili ninla kwanza kufanyika baini ya Tanzania na DRC na limeandaliwa na Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa kushirikiana na Wizara ya Posta na Mawasiliano ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.