Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

TANZANIA YAJIFUNZA UENDESHAJI WA SATELITE NCHINI CHINA


Na Mwandishi Wetu, China

Wataalam wa masuala ya Mawasiliano kutoka Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari wamefanya ziara ya mafunzo nchini China kuhusu Uendeshaji wa Satelaiti yaliyoandaliwa na Kampuni ya China Great Wall Industry Corporation. 

Wataalamu hao wakiongozwa na Katibu  Mkuu wa Wizara hiyo, Bw. Mohammed Khamis Abdulla wamefanya ziara hiyo leo tarehe 27 Mei, 2024 kufuatia mwaliko wa Kampuni ya China Great Wall Industry Corporation (CGWIC) ambao ni wazoefu wa Uendeshaji wa Satelaiti.

Akitoa maelezo ya ukaribisho mwenyekiti wa Kampuni ya CGWIC Bw. Hu Zhongmin amesema kuwa wako tayari kuisaidia Tanzania katika hatua zote kuanzia uundaji wa Satelaiti hadi uendeshaji wake.

Naye Bw. Abdulla ameishukuru Kampuni ya CGWIC kwa niaba ya Serikali ya Tanzania kwa utayari waliouonesha wa kuisaidia Tanzania katika masuala ya Satelaiti hasa katika kipindi hiki ambapo Tanzania na China zinasherehekea miaka 60 ya ushirikiano wa kidiplomasia ulioanza mwaka 1964.