Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

TANZANIA YAJIFUNZA KUTOKA JIPDEC KUIMARISHA ULINZI WA TAARIFA NA MIFUMO YA KIDIJITALI


Na Mwandishi Wetu, WMTH, Osaka

Mkurugenzi wa Mawasiliano kutoka Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Bw. Mulembwa Munaku (wa tatu kutoka kushoto), ameongoza ujumbe wa wataalam wa Serikali ya Tanzania waliotembelea Taasisi ya Kukuza Uchumi wa Kidijitali na Jamii ya Japan (Japan Institute for Promotion of Digital Economy and Community – JIPDEC) kwa lengo la kupata uzoefu katika eneo la ulinzi wa taarifa binafsi na kuimarisha mifumo ya utawala bora wa kidijitali.

Bw. Munaku amesema kuwa Tanzania inalenga kujifunza kutokana na uzoefu wa JIPDEC katika kujenga jamii salama, yenye kuaminika na inayounganishwa kimataifa kwa njia ya kidijitali. Ameongeza kuwa kupitia majadiliano hayo, pande zote mbili zitaendelea kushirikiana katika kuimarisha utaalamu wa usimamizi na tathmini ya usalama wa taarifa na mifumo ya kidijitali, ikiwemo huduma za wingu (cloud-based solutions) na majukwaa yanayounganisha taasisi mbalimbali za Serikali.

Kwa upande wake, Rais wa JIPDEC, Bw. Hideji Sugiyama, amesema taasisi hiyo imejiimarisha katika maeneo mbalimbali ikiwemo Mfumo wa Alama ya Faragha (PrivacyMark System), Mfumo wa Usalama wa Taarifa (ISMS), pamoja na kufanya tafiti kuhusu masuala ya faragha na uchumi wa kidijitali katika ngazi ya kitaifa na kimataifa. 

Pia ameongeza kuwa JIPDEC inasimamia Msimbo wa Kampuni wa Kiwango (Standard Company Code) unaotumika kutambua kampuni kwa nambari maalumu, na inashirikiana na serikali, sekta binafsi na taasisi za elimu katika kutoa mapendekezo ya sera za kuimarisha matumizi salama ya teknolojia za kidijitali.

Taasisi ya JIPDEC, iliyoanzishwa mwaka 1967, ni taasisi isiyo ya kiserikali inayolenga kukuza uchumi wa kidijitali na jamii yenye taarifa salama na za kuaminika. Kwa kipindi chote cha zaidi ya miaka 50, imeendelea kubadilika sambamba na maendeleo ya teknolojia, na kuendelea kuwa nguzo muhimu katika ukuaji wa uchumi wa kidijitali nchini Japani.

Kupitia ushirikiano huu, Tanzania inatarajia kuboresha uwezo wa kusimamia taarifa kwa usalama, kuongeza uaminifu wa kidijitali, na kuhakikisha huduma za serikali mtandaoni zinakuwa jumuishi, salama na zenye kuaminika kwa wananchi na wadau wake.

Ziara hiyo ilifanyika pembezoni mwa Maonesho ya Osaka, ikiwa ni sehemu ya Wiki ya Sayansi na Teknolojia, ambapo nchi mbalimbali duniani zinashiriki, na inatarajiwa kumalizika tarehe 13 Oktoba, 2025.