Habari
TANZANIA YAIMARISHA USHIRIKIANO WA KIMKAKATI NA IRAN KATIKA TEHAMA NA UBUNIFU WA KIDIJITALI
Na Mwandishi Geneva, Uswisi
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran zimekubaliana kuimarisha ushirikiano wa kimkakati katika Sekta ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), hatua inayolenga kuharakisha mageuzi ya kidijitali, kukuza ubunifu na kujenga uwezo wa wataalamu ili kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Makubaliano hayo yalifikiwa katika kikao kati ya Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari wa Tanzania, Mhe. Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki, na Naibu Waziri wa TEHAMA wa Iran ambaye pia ni Mkuu wa Shirika la TEHAMA la Iran, Dkt. Mohammad Mohsen Sadr, kilichofanyika mjini Geneva, Uswisi.
Akizungumza katika kikao hicho, Mhe. Kairuki alisema Tanzania inaendelea kutekeleza ajenda ya mageuzi ya kidijitali kupitia upanuzi wa miundombinu ya mawasiliano, huduma za serikali mtandao, usalama wa mtandao, ulinzi wa taarifa binafsi na matumizi ya teknolojia zinazoibukia kama Akili Unde (AI).
Alisema Tanzania iko tayari kushirikiana na Iran katika utafiti wa AI, usalama wa mtandao, ubunifu, mafunzo ya wataalamu na kubadilishana uzoefu kati ya taasisi za TEHAMA za nchi hizo mbili.
Aidha, Mhe. Kairuki alipendekeza kuandaliwa kwa Hati ya Makubaliano (MoU) kati ya Tanzania na Wizara husika ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ili kuweka msingi wa ushirikiano wa muda mrefu na kurahisisha utekelezaji wa programu za pamoja.
Kwa upande wake, Dkt. Sadr alisema Iran iko tayari kushirikiana na Tanzania kwa kushirikisha uzoefu wake katika mageuzi ya kidijitali, mifumo ya serikali kidijitali, usalama wa mtandao, majukwaa ya kidijitali, kampuni bunifu (startups), pamoja na kuunganisha sekta binafsi za nchi hizo mbili katika uwekezaji na ubunifu wa teknolojia.
Dkt. Sadr pia aliahidi kuwa Iran itaiwasilisha kwa Tanzania rasimu ya awali ya Hati ya Makubaliano (MoU) ndani ya mwezi mmoja, huku pande zote zikisisitiza dhamira ya kuendeleza ushirikiano huo kupitia mafunzo, ziara za kitaalamu na utekelezaji wa miradi ya pamoja katika TEHAMA na ubunifu wa kidijitali.
