Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

Tanzania yahimiza Matumizi ya Akili Unde katika Ukanda wa Afrika Mashariki


Tanzania imehimiza nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kuongeza juhudi za pamoja katika utafutaji wa rasilimali fedha za kuendesha programu mbalimbali ikiwemo utafiti na ujenzi wa miundombinu ya kidijitali, kubadilishana maarifa, kukuza ubunifu wa ndani na kuendeleza miradi ya pamoja ya Teknolojia ili kujenga uthibiti wa kiuchumi na kijamii katika Jumuiya.

 

Rai hiyo imetolewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Mahmoud Thabit Kombo (Mb), wakati akitoa salamu za Tanzania katika Kongamano la Nne la Sayansi, Teknolojia na Ubunifu la Jumuiya ya Afrika Mashariki lililoandaliwa na Kamisheni ya Sayansi na Teknolojia ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EASTECO) kwa kushirikiana na Bazara la Vyuo Vikuu la Jumuiya ya Afrika Mashariki (IUCEA), linalofanyika jijini Kigali, Rwanda kuanzia tarehe 30 Machi hadi 1 Aprili 2026.

 

Kongamano hilo linaloongozwa na kauli mbiu isemayo “Matumizi ya Akili Unde kwa ajili ya Afrika Mashariki yenye Ustahimilivu, Jumuishi na Ubunifu” liliwakutanisha viongozi wa ngazi za juu wa Serikali kutoka nchi wanachama wa EAC, wabunifu, wanataaluma, wanadiplomasia na wadau wa maendeleo pamoja ya mashirika mbalimbali ya Kimataifa.

 

Katika Kongamano hilo, Ujumbe wa Tanzania uliongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Mahmoud Thabit Kombo aliyeambatana na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Prof. Adolf Mkenda, Katibu Mkuu Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Bw. Mohammed Khamis Abdulla, Kaimu Katibu Mkuu anayesimamia masuala ya Afrika Mashariki kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Said Shaib Mussa, Maafisa Waandamizi wa Wizara na Taasisi za Serikali pamoja na Wanataaluma kutoka Taasisi za  mbalimbali za Elimu ya Juu nchini.

 

Akizungumzia mchango wa Tanzania, Waziri Kombo alieleza kuwa Tanzania chini ya uongozi wa Rais Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeweka kipaumbele katika kukuza sekta za Teknolojia, Uchumi wa Kidijitali na Ubunifu kama nguzo muhimu za agenda ya maendeleo ya Taifa na Dira ya Maendeleo ya 2050.

 

Mbali na hayo Waziri Kombo aligusia umuhimu wa kuweka mifumo thabiti ya sera na udhibiti na utoaji elimu ili kuhakikisha matumizi salama na yenye maadili ya Akili Unde. Aliongeza kuwa pasipo kuwa na usimamizi madhubuti teknolojia hiyo inaweza kuongeza changamoto katika jamii ikiwemo tishio la usalama na kukithiri kwa tofauti ya kiuchumi.