Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

TANZANIA YAANZA MAZUNGUMZO NA CHINA KUHUSU USHIRIKIANO KATIKA TEKNOLOJIA YA ANGA ZA JUU


Na Juma Wange, WHMTH, Dodoma.

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imeanza mazungumzo na Shirika la Sayansi na Teknolojia la Anga la China (CASC) kwa ajili ya kushirikiana katika Teknolojia ya Anga za Juu ‘Satellite’ (Space Technology) na Ulinzi wa Taarifa Binafsi (Data Protection). 

Mazungumzo hayo yamefanyika leo tarehe 27 Juni 2023 kwa njia ya video mkutano (video conference) na kushirikisha uongozi wa Wizara akiwemo Mhe. Waziri Nape Moses Nnauye (Mb); Katibu Mkuu Mohammed Khamis Abdulla; Naibu Katibu Selestine Gervas Kakele na viongozi wengine wa Wizara na Taasisi zake - Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA); Mfuko wa Mawasiliano Kwa Wote (UCSAF); Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL); Tume ya TEHAMA Tanzania (ICTC); na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC). 

Kwa upande wa China, mazungumzo yalihusisha ushiriki wa Mhe. Mbelwa Kairuki, Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini China; Mwenyekiti wa Shirika CASC Bw. Hu Zhongmin; wakiwemo pia viongozi  mbalimbali wa Shirika hilo.
 
Mazungumzo hayo ni hatua nyingine ya Serikali ya kuwa na mikakati endelevu ya kujenga na kukuza uchumi wa kidijitali wenye kuleta tija na maisha bora kwa kila Mtanzania kupitia TEHAMA. 

Tanzania na China zimekuwa na mahusiano ya kihistoria kwa muda mrefu katika nyanja mbalimbali za maendeleo ikiwa ni pamoja na uchumi, siasa, utamaduni, diplomasia na michezo.